Rais John Magufuli leo Agosti 24 amemuapisha Brigedia Jenerali John Mbungo kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Hafla ya kuapishwa kwa Brigedia Mbungo imefanyika Ikulu na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma.
Pia alikuwapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Anjellah Kairuki, Waziri wa Sheria na Katiba Prof. Palamagamba Kabudi na Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Pamoja na kula kiapo hicho , Brigedia Mbungo amekula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Harold Nsekela.
Rais Magufuli amewataka viongozi wote nchini kushirikiana katika jukumu la mapambano dhidi ya rushwa ili kuepusha madhara ya tatizo hilo katika uchumi na ustawi wa jamii.
“Ukiangalia mambo makubwa tunayopambana nayo yanasababishwa na rushwa iliyosambaa kila mahali, watumishi hewa chanzo ni rushwa, dawa za kulevya ndani yake kuna rushwa, vyeti feki ndani kuna rushwa, mikataba mibovu ndani kuna rushwa, pembejeo za ruzuku ndani kuna rushwa na huko mahakamani nako ni rushwa tu” amesisitiza Rais Magufuli.
‘’Tukifanikiwa kupunguza rushwa kwa angalau asilimia 80, nchi yetu itafanikiwa kutatua matatizo mengi, na ni vema mtambue kuwa hatua hizi tunazochukua zimeanza kuwavutia wafadhili wengi na wawekezaji’’amesema
“Na mimi nikiwa kiongozi wenu nimeamua kupambana na rushwa kikwelikweli, na ninawaomba nyote mshirikiane kuondoa rushwa katika maeneo yenu ya kazi” amefafanua Rais Magufuli.
Brigedia Mbungo ameshukuru kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo na ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wengine wa taasisi hiyo katika mapambano dhidi ya rushwa.
No comments:
Post a Comment