Kesi mmiliki wa Lucky Vicent bado nzito

Mahakama ya ya Wilaya ya Arumeru imehairisha kesi inayomkabili mmiliki wa Shule ya Lucky Vicent, Innocent Moshi hadi Septemba 11 mwaka huu huku Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Desdery Kamugisha akitoa onyo kwa Jamhuri iweze kukamilisha hoja za awaliAkitoa onyo hilo amesema kesi hiyo ilifika Mahakamani hapo tokea Mei 12 mwaka huu na rekodi zinaonyesha upelelezi umekamilika, hivyo endapo hoja za awali hazitasomwa tarehe iliyotajwa ya kusikiliza kesi hiyo, Mahakama itachukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria na haitaahirisha tena.

Akizungumza Mahakamani hapo Wakili wa serikali, Khalili Nuda aliiomba Mahakama kuahirisha kesi hiyo ili wakamilishe kuandaa hoja za awali ambazo kwa sasa bado hawajaziandaa. Ambapo kwa upande wake Wakili wa Utetezi Method Kimomogolo ameiomba Mahakama hiyo kuahirishwa kwa mara ya mwisho kwa kesi hiyo.

Awali wakisomewa mashitaka yao Mei 12, mwaka huu na Mwanasheria wa serikali, Rose Sulle alisema Mahakamani hapo kuwa  washtakiwa  hao walitenda makosa hayo Mei 6 mwaka huu, katika eneo la Kwa Morombo jijini Arusha.

Sulle amedai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa wa kwanza anadaiwa  mnamo Mei 6 eneo la kwa Morombo  akiwa mmiliki wa gari aina ya Toyota Rosa lenye namba za usajili T.871 BYS, alimruhusu dereva wake kuendesha gari la abiria  kwenye barabara ya umma bila ya kuwa na leseni ya usafirishaji jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Mwanasheria wa serikali, Sulle amesema katika shitaka la pili Moshi anadaiwa kuruhusu gari hilo kuendeshwa bila kuwa na bima na shitaka la tatu ni kushindwa kuwa na mkataba na dereva wake ambaye kwa sasa ni marehemu Dismas  Gasper.
Mmiliki huyo wa Lucky Vicent alisomewa shitaka la  nne  analodaiwa kuruhusu gari lake kubeba abiria waliozidi uwezo wa gari ambapo abiria 13 walizidi.

Wakili huyo wa serikali akisoma shitaka mwalimu Mkama, alidai kuwa akiwa na nafasi ya Mwalimu Mkuu Msaidizi  na mwandaaaji wa safari hiyo aliruhusu kupakia abiria zaidi ya 13 kwenye gari liliosababisha vifo vya watu 35.

Washitakiwa hao walikana mashitaka yao ambapo washitakiwa hao wapo nje baada ya kukidhi masharti ya dhamana yaliyowataka wawe na wadhamini wawili wenye vitambulisho na kusaini hati ya shilingi  Milioni 15 kwa kila mmoja na kutosafiri nje ya mkoa wa Arusha mpaka kesi hiyo itakapomalizika mahakamani hivyo wakatakiwa kukabidhi hati za kusafiria mahakamani hapo.

Mnamo Mei 6, mwaka huu wanafunzi 32 ,walimu wawili na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent waliofariki kwa ajali eneo la Rhotya ,wakielekea mjini Karatu katika shule ya msingi Tumaini kufanya mtihani wa ujirani mwema.


Kesi mmiliki wa Lucky Vicent bado nzito Kesi mmiliki wa Lucky Vicent bado nzito Reviewed by KUSAGANEWS on August 24, 2017 Rating: 5

No comments: