Mahakama Kuu Kanda ya Rukwa leo imewahukumu kwenda jela miaka 20, watuhumiwa nane kati ya tisa waliokutwa na hatia katika kesi mbili tofauti zinazohusiana na jaribio la kutaka kuwaua watu wawili wenye ualbino, huku mmoja akihukumiwa miaka 14.Hukumu hiyo imetolewa leo Agosti 31, ambapo kesi ya kwanza iliwahusu watuhumiwa 10 ambao wanadaiwa kula njama ya kumshambulia na kujaribu kumuua mtoto Mwingulu Matomange mnamo mwaka 2013.
Katika kesi hiyo ya Matomange ambaye wakati tukio hilo lilipofanyika, alikuwa na umri wa miaka 7, watuhumiwa walikuwa 10, huku wanne wakiachwa huru na sita wakiwekwa ndani ya nondo kwa miaka 20, kila mmoja.
Kesi ya pili iliwahusu watuhumiwa wanne waliodaiwa kumshambulia Maria Chambanenge aliyekuwa na miaka 39, wakati uhalifu huo ukitekelezwa mwaka huo huo wa 2013.
Katika kesi hiyo watuhumiwa wawili wamehukumiwa kwenda jela miaka 20, kila mmoja na mmoja kuhukumiwa kifungo cha miaka 14, huku mwingine akiachwa huru. Pamoja na hayo watuhumiwa hao wanadaiwa kukutwa na mikono ya waathirika hao ambao wote wana ulemavu wa ngozi.
No comments:
Post a Comment