JUMBE ZA AMANI ZATAWALA MKUTANO WA JUBILEE UWANJANI UHURU PARK

MRENGO wa serikali ya Jubilee unaoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto Ijumaa umefanya umeandaa mkutano mkubwa wa kujipigia debe Ijumaa uwanjani Uhuru Park, Nairobi.

Kwenye hafla hiyo ya kampeni za mwisho Kaunti ya Nairobi, kando na kunadi sera zake vinara wa mrengo huu waliohutubu wamehubiri na kueneza jumbe za amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu unaosubiriwa kwa hamu na hamamu mnamo Jumanne, Agosti 8, 2017.

Kinara wa Jubilee Rais Kenyatta ameusuta muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa) akihoji kuwa unafaa kuhubiri amani badala ya kutishia wapinzani wao ambao ni Jubilee wanapoendesha kampeni zao.

"Naskia huzuni nikiona wenzetu wakienda mahali wanaeleza watu waondoke. Hii ni Kenya yetu, jamani waondoke waende wapi?" akataka kujua kiongozi huyu wa taifa.

Alikuwa akirejelea matamshi ya kinara wa Nasa Raila Odinga ya awali akiwa katika Kaunti ya Kajiado alipozungumza kuhusu jinsi ya kutatua swala la ardhi kwa jamii zinazoishi maeneo hayo endapo ataibuka mshindi.

Hata hivyo Raila alisema kuwa matamshi yake yalitafsiriwa vibaya, jambo ambalo lilizua tumbo joto miongoni mwa viongozi katika Jubilee.

Rais aidha amewashauri vijana kutokubali kutumiwa na wanasiasa kuzua fujo na ghasia msimu wa uchaguzi. "Vijana ninawaomba msikubali kuchochewa na wanasiasa mzue ghasia. Anayewaeleza muende mpigane watoto wake wako salama. Tupige kura na tuishi kwa amani," akashauri.

"Haja yetu si matusi ila kufanya maendeleo ya kukuza taifa hili. Hatuna haja za kutusi wapinzani wetu, haja yetu ni kazi. Hata wakitutusi, mimi huwaeleza tulizeni boli tufanye kazi," akaongeza akionekana kulenga vinara wa Nasa.

Nasa inaongoza na mpeperusha bendera yake ya urais Raila Odinga (ODM), mgombea mwenza Kalonzo Musyoka (Wiper Partu), Seneta Moses Wetangula (Ford-Kenya), Musalia Mudavadi (ANC) na Gavana Isaac Rutto (Chama Cha Mashinani/CCM).

Alisuta Nasa akisema kuwa hawana ajenda za maendeleo ya nchi hii licha ya kuwa wanataka kuiongoza. "Wenzetu kwa sababu hawajui maendeleo, wanataka watu waishi kwa umaskini. Walianza kuharibu mambo kwa kuingilia kila miradi tunayofanya," akasema akitaja mradi wa reli ya kisasa ya SGR.

Nasa imekuwa ikisuta Jubilee kwa mradi huo uliogharimu sh327 bilioni kwamba ulibuniwa na Raila na Rais Mstaafu Mwai Kibaki, wakati akiwa Waziri Mkuu chini ya serikali ya mseto.

Imekuwa ikihoji uligharimu sh100 bilioni zaidi kinyume na zabuni ya awali.

Kalonzo alikuwa Makamu Rais wa Rais Kibaki.

Rais Kenyatta aidha amejipigia debe akirejelea miradi ya maendeleo aliyotekeleza akiwa mamlakani kwa kipindi cha miaka minne iliyopita akitaja uzazi wa bila malipo kama hatua kubwa ambayo taifa imepiga mbele kando na miradi mingine.

"Hakuna mtoto atakaa nyumbani kwa sababu amekosa karo, mwaka ujao kuanzia chekechea hadi kidato cha nne shule za serikal elimu itakuwa ya bure. Kazi ya mzazi itakuwa kujifungua mtoto na kukaa raha mustarehe akifahamu fika kuwa uzazi hauna malipo na elimu ni bure," akaeleza akiuza ajenda za Jubilee, akiongeza kuwa wanawake wajawazito watapewa kadi za bima ya afya (NHIF) kuanzia mwaka ujao.

Kiongozi huyu ametumia fursa hiyo kupigia debe wawaniaji wa viti mbali mbali vya kisiasa Nairobi kwa tiketi ya Jubilee.

"Mtatupa Gavana, Seneta, Mwakilishi wa Wanawake, Wabunge na Madiwani (MCA's) wanaoelewa shida za Nairobi?" akauliza Rais akiwafanyia kampeni akiwemo Seneta Mike Sonko anayewania ugavana Nairobi na mbunge Maalumu Johnson Sakaja anayemezea mate kiti cha useneta, wote kwa chama cha Jubilee.

Sonko atapambana na Gavana wa sasa Nairobi Dkt Evans Kidero wa ODM anayewania kukihifadhi.

"Agosti 8 mjitokeze kwa wingi tumpeleke huyu mtu wa kitendawili nyumbani asubuhi na mapema," akawarai akilenga Raila.

Naibu Rais Ruto pia amekuwa na ule ujumbe mmoja wa amani. "Mnataka ule mtu wa vitendawili atuletee hadithi? Sisi tunataka amani. Wenzetu tunaoshindana nao wamekuwa wakiandamana mitaani na kuenda kortini. Mara hii ili wasiende kortini tuwashinde kwa zaidi ya kura milioni 3," akasema Ruto akiuza ajenda za Jubilee.

"Wawache kutueleza mambo ya wizi wa kura. Wao ndio walisema hawana imani na makamishna wa IEBC wa hapo awali, si waliondoka? Tunawaambia korti hazitapiga kura, karatasi za kura hazitapiga kura, IEBC haitapiga kura. Wananchi wa Kenya ndio watapiga kura," akasuta Nasa.

Imani

Nasa ilieleza kuwa haina imani na maafisa wa awali wa tume huru ya uchaguzi na mipaka walioongoza uchaguzi wa mwaka wa 2013 chini ya mwenyekiti wake Isaack Hassan, hivyo basi wakaondolewa na kupisha Bw Wafula Chebukati (Mwenyekiti) na makamishna wengine kuchukua hatamu ya kusimamia na kuendesha uchaguzi wa mwaka huu wa 2017.

Naibu Rais pia ameonekana kupigia debe wawaniaji wa viti vya kisiasa Jubilee Kaunti ya Nairobi.

Jubilee inatarajiwa kufanya kongamano la mwisho kesho Jumamosi katika uwanja wa Afraha mjini Nakuru ambapo litakuwa la mwisho kufanya kampeni, kwa mujibu wa kanuni za IEBC mirengo ya kisiasa kutamatisha kampeni zao siku mbili kabla uchaguzi ufanyike.

Ni katika ugani wa Afraha ambapo baada ya Jubilee kuibuka mshindi uchaguzi mwaka wa 2013 walifanyia maombi ya kitaifa kumshukuru Mungu na wapiga kura kwa ufanisi wao.

JUMBE ZA AMANI ZATAWALA MKUTANO WA JUBILEE UWANJANI UHURU PARK JUMBE ZA AMANI ZATAWALA MKUTANO WA JUBILEE UWANJANI UHURU PARK Reviewed by KUSAGANEWS on August 04, 2017 Rating: 5

No comments: