JUBILEE YA ODINGA HAPATOSHI.

MUUNGANO wa Upinzani, NASA, umedai Serikali ya Jubilee inatoa vitisho kwa viongozi wa upinzani walioshindwa kwa njia tatanishi ili wakubali matokeo ya uchaguzi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni za Kitaifa katika NASA, Bw Musalia Mudavadi, Jumatatu alisema wengi wanaolengwa ni waliokuwa wakitetea viti vyao vya ugavana katika uchaguzi mkuu.

“Wengi wao walikuwa wamepanga kupinga matokeo mahakamani ili ushindi wa wapinzani wao ufutiliwe mbali,” akasema kwenye taarifa wa vyumba vya habari.

Muungano huo ulikuwa umedai kulikuwa na wizi wa kura katika kaunti kadhaa zikiwemo Garissa, Machakos, Nairobi, Narok, Kajiado, Wajir na Marsabit ambako washindi wa Jubilee walipata asilimia ya kura zilizokaribia kufanana sana.

Katika Kaunti ya Machakos, Dkt Alfred Mutua, wa Chama cha Maendeleo Chap Chap kilichomuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta, alishinda kwa asilimia 53.21 huku Bi Wavinya Ndeti, wa Chama cha Wiper kilicho ndani ya NASA akiibuka wa pili kwa asilimia 44.54 za kura.

Bw Mike Sonko, alishinda ugavana Kaunti ya Nairobi kwa asilimia 53.48 dhidi ya aliyekuwa Gavana Dkt Evans Kidero, wa Chama cha ODM aliyepata asilimia 42.87.

Chama cha Jubilee kilishinda ugavana pia Narok na Kajiado kupitia kwa Bw Samuel Tunai (asilimia 52.23) na Bw Joseph ole Lenku (asilimia 53.76).

Katika kaunti hizo mbili, Bw Keturet ole Ntutu, wa Chama Cha Mashinani kilicho tanzu cha NASA, na David Nkedianye, wa ODM waliibuka wa pili kwa asilimia 33.3 na asilimia 45.05 mtawalia.

“Serikali inajua kila kesi mahakamani itafichua ulaghai wake kwa hivyo inafanya kila juhudi, ikiwemo vitisho, ili ikubaliwe na kuidhinishwa kama serikali halali,” akasema Bw Mudavadi.

Mbali na viongozi walioshindwa, Kiongozi huyo wa Chama cha Amani National Congress (ANC) alizidi kudai kwamba wanachama wa upinzani walioshinda wanalazimishwa kutangaza watashirikiana na Serikali ya Jubilee.

Kulingana naye, miongoni mwa vitisho vinavyotolewa ni kuwafungulia wanasiasa hao mashtaka mbalimbali, ukaguzi wa rekodi zao za ushuru kwa njia inayovuka mipaka, na kutatiza biashara zao.

“Hatua hizi si tofauti na mashambulio haramu yaliyofanywa dhidi ya mashirika ya kijamii na uharibifu wa vituo vya kuhesabu kura vya NASA katika wiki chache zilizopita,” akasema.

Dkt Kidero alikuwa miongoni mwa magavana waliotarajiwa kupinga matokeo ya uchaguzi, lakini jana akahudhuria hafla ya kuapishwa kwa Bw Sonko, akakubali kushindwa na akajitolea kumshauri gavana huyo mpya endapo atahitaji usaidizi wowote.

Rais Kenyatta ambaye alihudhuria hafla hiyo alimsifu kwa hatua yake na kusema imeonyesha ukomavu wa kisiasa.

JUBILEE YA ODINGA HAPATOSHI. JUBILEE YA ODINGA HAPATOSHI. Reviewed by KUSAGANEWS on August 21, 2017 Rating: 5

No comments: