JPM, Museveni wasubiriwa Tanga wakikumbushwa fidia

 Ikiwa ni takriban mwezi mmoja baada ya mkataba wa ujenzi wa bomba la mafuta kusainiwa mjini Kampala, Uganda, uzinduzi wa ujenzi huo unatarajiwa kufanywa Julai 15 mjini Tanga na marais John Magufuli na Yoweri Museveni wa Uganda.

Hata hivyo, wakati zikiwa zimebaki siku tano kufikia siku yenyewe, wananchi wamewatuma salamu wakuu hao wa nchi wakitaka malipo ya fidia za maeneo yao. Mkataba wa ujenzi wa bomba hilo linaloanzia Hoima, Uganda hadi mjini hapa ulisainiwa Mei 26 na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Waziri wa Nishati wa Uganda, Irene Muloni.

Akizungumza na wananchi juzi, mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella alisema marais hao wataweka jiwe la msingi katika kata ya Chongoleani.

Hata hivyo, wananchi wa eneo hilo walisema kabla ya marais hao kuwasili ni vyema walipwe fidia ya mali na ardhi iliyochukuliwa na wahakikishiwe ulinzi na usalama kutokana na matarajio ya kuwapo kwa idadi kubwa ya wageni.

Pia, walitaka wawekewe mazingira bora ya uvuvi wa kisasa.

“Sisi wakazi wa Chongoleani ni watulivu na hatuna maneno kuhusu huu mradi, lakini unawezaje kuanza ujenzi bila kulipa fidia? Hatuna raha kuhusu hili, isije nchi ikaingia aibu kwa marais watakapopokewa kwa mabango ya kulalamikia fidia,” alisema Omari Mustapha (70).

Mnungu Twaha (87), alisema pamoja na kuupokea mradi huo wakazi wa eneo hilo wana hofu ya kuingiliwa na makundi ya kihalifu, hivyo kuna haja kwa Serikali kuwahakikishia usalama.

Waziri Chuma alisema baada ya kuhisi hali ya usalama katika eneo hilo itakuwa tete kutokana na kuwasili wageni wasioeleweka, waliandaliwa vijana 150 ili wapewe mafunzo ya mgambo lakini ofisi ya mshauri wa mgambo Wilaya ya Tanga iliwataka kuchanga fedha za kuwalisha wawapo mafunzoni.

“Sisi vijana wa hapa tulifanya jitihada za kujikusanya, lakini ofisi ya mshauri wa mgambo inatoa masharti ya kutukwamisha. Tunaomba mkuu wa mkoa lichukue hili ili kuimarisha ulinzi wa hapa, kwani tunatambua kuwa ulinzi wa hapa utatuhusu sisi wenyewe,” alisema Chuma.

Mkuu wa mkoa, Shigela aliwatoa hofu wakazi wa eneo hilo kwa kuwahakikishia kuwa fidia itatolewa kwa kila atakayeguswa na mradi huo na kuwaomba kuwa na subira wakati mchakato unaendelea kufanyika.

“Mradi huu unapita katika eneo lenye urefu wa kilomita 1,400 kutoka Hoima hadi hapa Chongoleani, mchakato wake unahitaji umakini na uangalifu mkubwa ili kila mmoja apate fidia bila kupunjwa, na katika hili Serikali ipo imara,” alisema.


JPM, Museveni wasubiriwa Tanga wakikumbushwa fidia JPM, Museveni wasubiriwa Tanga wakikumbushwa fidia Reviewed by KUSAGANEWS on July 09, 2017 Rating: 5

No comments: