Katibu wa CCM wilaya ya Arusha mjini, Ramadhani Dallo amesema atawachukulia sheria wanachama wanaogombea nafasi mbalimbali ambao watagundulika kukiuka kanuni na sheria za uchaguzi.
Dallo ameyasema hayo leo wakati akizungumzia mchakato wa uchukuaji fomu kwa ajili ya kugombea nafasi mbalimbali ngazi ya wilaya.
Kanuni hizo ni pamoja na kutofanya kampeni, kutangaza nia au kujinadi kwa aina yoyote.
Zoezi la uchukuaji na urudishwaji fomu lilianza Julai 2 na litafungwa Julai 10.
“Katika kipindi hiki cha uchukuaji fomu na urudishwaji, wanachama pamoja na wagombea hao wanapaswa kufuata sheria na kanuni zote za uchaguzi zilizowekwa na yeyote atakayekiuka atachukuliwa sheria kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.”amesema
Hivyo aliwataka wanachama wa chama hicho pamoja na wagombea kuendelea kufuata taratibu hizo kwani mgombea yeyote atakayegundulika kukiuka taratibu atakuwa amejiondoa wenyewe .
Dallo alizitaja nafasi zinazogombewa kuwa ni Mwenyekiti wa wilaya, Katibu Siasa na Uenezi wa Wilaya, Mjumbe wa Halmashauri Kuu wilaya nafasi 10, Mjumbe Mkutano mkuu mkoa nafasi mbili,Mjumbe wa Mkutano mkuu Taifa nafasi tatu na Mjumbe wa Halmashauri Kuu Mkoa, nafasi mbili.
Amesema mwamko ni mkubwa sana kwa wanachama wanaowania nafasi mbalimbali katika chama hicho.
"Kwa kweli watu wana mwamko sana wa kugombea nafasi mbalimbali na tunaendelea kuwaomba wajitokeze kwa wingi kwani kila mtu ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa,” amesema Dallo.
No comments:
Post a Comment