Uteuzi wa Miss Tanzania namba
mbili wa mwaka 2006, Jokate Mwegelo kuwa Kaimu Katibu wa Uhamasishaji wa Umoja
wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, unaonekana kutaka kuivuruga
jumuiya hiyo.
Mjadala mkubwa umeibuka kuhusu
uteuzi huo, ambapo baadhi ya wanachama na viongozi wa juu wa jumuiya hiyo
wamedai kuwa haukufuata kanuni na taratibu za umoja huo.
Vyanzo vya kuaminika kutoka katika
umoja huo vimedai kuwa baadhi ya viongozi wa juu wa UVCCM hawakushirikishwa
katika uteuzi huo uliofanywa na kigogo mmoja wa umoja huo.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa
uteuzi huo haukushirikisha wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji wala Baraza Kuu la
UVCCM, ambalo halikukutana kumthibitisha Jokate kama kanuni zinavyoelekeza.
Kwa mujibu wa kanuni za jumuiya
hiyo, wajumbe wa kamati ya utekelezaji hawazidi 10, ambapo miongoni mwao ni
Mwenyekiti wa umoja huo Taifa, Makamu Mwenyekiti Taifa, Katibu Mkuu, Naibu
Katibu Mkuu na mjumbe mmoja kutoka makao makuu ya chama.
Wajumbe wa baraza kuu ni wenyeviti
na makatibu wa mikoa na mjumbe mmoja kutoka katika kila mkoa.
Kutokana na kile kilichodaiwa kuwa
ni mvurugano ndani ya umoja huo, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Shaka Hamdu
Shaka, amesema kuwa uteuzi huo ulifuata taratibu zote za chama.
“Ni kweli amekaimishwa kwa kufuata
taratibu zote za chama, kikao cha Kamati ya Utekelezaji kilikutana Aprili 18,
mwaka huu, Dar es Salaam na ndicho kimewakaimisha wakuu wa idara watano akiwamo
Jokate.
“Hao wanaolalamika hawajui kanuni na
taratibu za jumuiya yetu, huwezi kupata nafasi kama kikao cha Kamati ya Utekelezaji
hakijakaa,” alisema Shaka.
Hata hivyo alikiri kutoitishwa kwa
kikao cha Baraza Kuu ili kuthibitisha uteuzi huo, akisema ni gharama kubwa
kuitisha kikao hicho.
“Kwa kawaida Baraza Kuu huwa
linakutana kila baada ya mwaka mmoja, kuita baraza kuu ni gharama sana hivyo
ikitokea kuna nafasi wazi Kamati ya Utekelezaji ina mamlaka pia ya
kumthibitisha,” alisema.
Kwa upande wake, Jokate alishukuru
kwa uteuzi huo na kuahidi kuifanya jumuiya hiyo iwe karibu zaidi na vijana wa
Kitanzania.
“Nashukuru kwa imani waliyoonyesha
viongozi wangu ila zaidi kuona nina uwezo wa kuongoza idara hiyo nyeti na
muhimu kwenye jumuiya.
“Kikubwa ni kuifanya jumuiya iwe
karibu zaidi na vijana wa Kitanzania na kurudisha tumaini na kusimamia
changamoto wanazozikabili vijana katika kujiletea maendeleo,”
alisema Jokate.
Jokate pia alikuwa miongozi mwa
wanachama 450 wa CCM waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge wa Bunge la
Afrika Mashariki (EALA).
Jokate alianzia kwenye mashindano ya
Miss Tanzania mwaka 2006 ambapo aliibuka mshindi wa pili.
Hivi sasa anajishughulisha na sanaa
na ujasiriamali ambapo anamiliki Lebo ya Kidoti Fashion inayojihusisha na
uuzaji wa nywele na mavazi.
Uteuzi wa Jokate Mwegelo UVCCM Waibua Mfarakano
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 24, 2017
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 24, 2017
Rating:


No comments:
Post a Comment