RAIS John Magufuli ametakiwa kufuta
posho zote zisizokuwa za lazima kwa wabunge huku watunga sheria hao
wakitakiwa kueleza waziwazi msimamo wao kuhusu kukataa posho hizo ili
fedha zitakazookolewa zitumike kwa kutatua changamoto mbalimbali
zinazowakabili wananchi katika majimbo yao.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na
Mwenyekiti wa Jukwaa Huru la Wazalendo, Ally Hapi wakati akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa wananchi kuunga mkono jitihada
zinazofanywa na Dk John Magufuli katika kupunguza matumizi yasiyo ya
lazima serikalini.
Hadi sasa wabunge ambao wamekataa
kupokea posho ya vikao vya Bunge ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto
ambaye akiwa katika Bunge la 10 akiwakilisha Jimbo la Kigoma Kaskazini
kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alitangaza
kutochukua posho akitaka zielekezwe kwa wapiga kura wake.
Mwingine ni Mbunge mpya wa Singida
Magharibi, Elibariki Kingu (CCM) aliyeandika barua kwa Katibu wa Bunge
huku akitoa msimamo wake kwamba hataki posho hizo, badala yake
zielekezwe jimboni kwake kusaidia changamoto mbalimbali zinazowakabili
wapiga kura wake.
Jana, katika akaunti yake ya Twitter,
Zitto aliandika kuwa, “Mshahara wa mbunge ni 3.8m kila mwezi. Posho ya
Ubunge 8m kwa mwezi. Posho ya kujikimu (perdiem) 120,000 kwa siku, kukaa
200,000 (posho ya vikao) kwa siku. Fedha za mfuko wa jimbo huwa around
48 mil kulingana na jimbo.
Sasa maposho yote hayo. “Mwambie mbunge
wako hizo posho apeleke jimboni kusaidia jamii, hizo ni kodi zetu mimi
na wewe. Kuna wabunge Majimbo yao hata matundu ya vyoo vya shule hamna
wakati laki moja tu yatosha.”
Mwenyekiti wa Jukwaa Huru la Wazalendo,
alisema wananchi pia wawasimamie wabunge wao waliowachagua katika
Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu ili waeleze msimamo wao
hadharani juu ya kuunga mkono hatua ya kukataa posho.
Alisema Jukwaa linatambua Dk Magufuli
ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kuidhinisha masharti ya kazi za
kibunge na stahiki wanazopaswa kulipwa katika kazi hiyo hivyo wanamuomba
kufuta kabisa posho kadhaa kwa wabunge.
“Tunamuomba Rais kufuta posho zote
zisizokuwa za lazima zinazolipwa kwa watumishi wa umma wa kada
mbalimbali yakiwemo mashirika ya umma,” alisema. Aliongeza kuwa wabunge
wote bila kujali vyama vyao waungane na Kingu pamoja na Zitto katika
kukataa malipo ya posho ili kupunguza mzigo mkubwa ambao serikali
inaubeba kuhudumia wabunge.
Kuhusu msimamo kwa wabunge, alisema
mbali ya kuwepo kwa wabunge wachache waliokataa kupokea fedha hizo ni
wakati sasa kwa wabunge wengine kueleza msimamo wao juu ya suala hilo.
“Jana (juzi), Mbunge wa Singida
Magharibi, Kingu aliandika barua kwa Katibu wa Bunge akieleza msimamo
wake wa kukataa kulipwa posho ya kitako ya Bunge katika kipindi chote
cha miaka mitano kuanzia 2015- 2020,” alisema Hapi.
Alisema mbunge huyo anakuwa wa pili
baada ya Zitto kutoka hadharani katika Bunge la 10 na kukataa posho hizo
ambazo msingi wake alidai ni unyonyaji wa wanyonge na ubadhirifu wa
kodi za wananchi.
Alisema Jukwaa hilo linapongeza maamuzi
ya Kingu na Zitto kwa ujasiri wake na uzalendo wake kwa taifa ikiwa ni
kuuunga mkono juhudi za Rais kwa vitendo wakitambua kuwa ubunge ni
utumishi na wala sio utukufu na kazi hiyo ni ya kuwawakilisha wananchi
na sio kuwanyonya.
“Jukwaa linatambua mapambano hayo
yaliyoanzishwa na Kingu yanahitaji kuungwa mkono na Watanzania wote
wanaoipenda nchi yao bila kujali itikadi za vyama,” alisema Hapi na
kuongeza kuwa baada ya msimamo wa Kingu, wapo wabunge wasiokuwa na
huruma hawakufurahishwa na hatua hiyo na wengine kuanza kumpigia simu na
kumtumia ujumbe mbalimbali.
Kwa upande wake, Katibu wa Jukwaa hilo,
Mtela Mwampamba alisema wataongoza vuguvugu lenye kuwaelimisha wananchi
pamoja na kufanya maandamano ili wabunge watoe msimamo wao ili kumuunga
mkono Rais Magufuli katika uamuzi aliochukua wa kubana matumizi ya
serikali.
mpekuzi blog
Wabunge Mtegoni: Rais Magufuli Aombwa Kufuta Posho za Zisizo na Umuhimu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
November 26, 2015
Rating:
No comments:
Post a Comment