Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na Ukawa, Edward
Lowassa jana kwa mara ya kwanza alikumbana na joto la upinzani baada ya msafara
wake kushambuliwa na mabomu ya polisi.
Tukio hilo, ambalo lilifanyika
mbele ya msafara wa Lowassa, lilitokea jana eneo la Daraja la Nduruma katika
Jiji la Arusha na kusababisha umati wa watu kutawanyika na wengine kutelekeza
magari yao.
Wakati Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
akimkaribisha kwenye chama hicho wakati wa mkutano mkuu alimwambia; “Mzee huku
inabidi uwe unafanya mazoezi kidogo, kuna mabomu huku.”
Lowassa alikumbwa na kadhia hiyo, akiwa njiani na
mgombea mwenza, Juma Duni Haji na viongozi wengine wa Ukawa, wakitokea Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), huku wakiwa wamesindikizwa na umati
wa watu na magari.
Tamko la polisi
Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
alisema kuwa polisi walilazimika kupiga mabomu ya machozi ili kutawanya watu
waliokuwa wakiwarushia mawe polisi na wengine kufunga barabara.
“Kwa hali ile, tungefanya nini? Wanatupa mawe kwa
polisi na wamefunga barabara na kuzuia magari mengine yasipite…ikumbukwe
kulikuwa hakuna kibali cha maandamano na hata kingekuja, matamko ya kuzuia
maandamano yameshatolewa,” alisema Sabas.
Katika tukio hilo, idadi kubwa ya polisi walikuwa
kwenye magari na silaha mbalimbali ambao baadaye walianza kurusha mabomu
kutawanya watu na magari kwa eneo la daraja hilo.
Hata hivyo, katika tukio hilo, lililotokea saa nane
mchana hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa na kutokana na nguvu hiyo ya polisi watu
walitawanyika, na barabara hiyo ya Arusha- Moshi ilifunguka baada ya kutopitika
kwa saa tano kuanzia saa nne asubuhi.
Ukawa walaani kupigwa mabomu
Akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa
Tindigani, Mbunge wa jimbo la Arusha, Godbless Lema alisema wamesikitishwa na
kitendo cha polisi kumpiga mabomu Lowassa na msafara wake.
“Tunajua polisi wamepata maelekezo na sasa wanataka
kuwatisha wananchi, lakini tunasema leo ndiyo mwisho hatutakubali tena
kunyanyaswa,” alisema Lema.
Kuwasili Lowassa
Lowassa aliwasili KIA saa 3:20 asubuhi akiwa
ameongozana na viongozi wa Ukawa, Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James
Mbatia na Mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi, Kaimu Mwenyekiti wa CUF taifa,
Twaha Taslima na viongozi wengine.
Kwenye Uwanja wa KIA, shughuli mbali mbali zilisimama
katika eneo la kushuka viongozi mashuhuri (VIP), ambapo mawaziri kadhaa
walikuwa katika eneo hilo.
Baadhi ya viongozi hao ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Hassadi, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais, Dk Mary Nagu, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tzeba.
Baada ya Lowassa kutua KIA, alikwenda moja kwa moja
kwenye Hoteli ya KIA Lodge na mgombea mwenza wake, Juma Duni Haji kwa mapumziko
mafupi.
Baada ya kupumzika saa 5:30 msafara ulianza kuelekea
uwanja wa Tindigani Kimandolu na ulifika saa tisa na kukutana uwanja ukiwa
tayari umefurika maelfu ya watu.
Akihutubia mkutano huo Lowassa alitahadharisha
viongozi wa polisi, kuacha kutumia nguvu kupita kiasi, kwani anaweza
kuwafikisha Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) iliyopo The Hague nchini
Uholanzi.
Lowassa alisema alikuwa akiiamini polisi, lakini
alichokiona jana cha kupigwa mabomu ni jambo baya.
Kuhusu suala la Babu Seya aliyefungwa kifungo cha
maisha gerezani alisema atafuatiliwa kwa kutumia suala la utawala bora kwa
kuangalia vyombo vya sheria na hatua zingine zitafuatwa.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema wanachama
wanaojiunga sasa wana haki sawa na mwasisi wa chama hiki Edwin Mtei mwenye kadi
namba moja.
Alisema mara baada ya wanachama wapya kujiunga, kwa
kipindi cha wiki moja nilipokea matusi mengi kuliko niliyowahi kutukanwa baada
ya kupokea wanachama wapya.
Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Taslima alisema kuna watu
ambao wamejenga desturi ya kuwabeza watu wanapohama vyama kwa hiari kwa kuwaita
oili chafu au makapi anavunja Katiba.
Alisema Ibara ya 20 ya Katiba ya mwaka 1977 inasema
kila mtu yeyote ambaye ni Mtanzania, yuko huru kujiunga na mtu yeyote, chombo
chochote, taasisi yoyote atakayopenda na hatazuiliwa.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema;
“Mabomu yamepigwa katika mkutano wa Chadema, watu wakafa Arusha, Arusha
tunayoitegemea kwa uchumi leo hii zaidi ya asilimia 19 ya pato ya taifa
linatokana na utalii, lakini leo (jana) tunaingia Arusha alipozaliwa Lowassa
tunapigwa mabomu, ukweli utatuweka huru.
Msafara wa Lowassa wapigwa mabomu Mto nduruma wakati anatokea katika viwanja vya KIA
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 16, 2015
Rating:
No comments:
Post a Comment