Baraza Kuu la Chadema limeridhia Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa apumzike wakati chama hicho kikiendelea na mchakato wa Uchaguzi Mkuu baada ya kiongozi huyo kutofautiana nao katika uamuzi wa kumkaribisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Baraza hilo jana
lilipiga kura ya wazi huku likishauri kuwa endapo atafikiria kubadili
uamuzi wake, atarejea kuendeleza safari ya chama hicho kuelekea Ikulu
chini ya mwavuli wa Ukawa.
Uamuzi huo ulifikiwa jana
wakati wa kikao cha Baraza Kuu kilichofanyika hapa baada ya Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe kueleza tofauti iliyojitokeza mwishoni mwa
mchakato wa kumpokea Lowassa baina ya Dk Slaa na Kamati Kuu kiasi cha
kumfanya Katibu Mkuu huyo kutohudhuria baadhi ya shughuli muhimu za
chama.
Mbowe alisema Kamati Kuu ilifanya vikao kadhaa
kutafakari ujio wa Lowassa na mashauriano ya muda mrefu ambayo hayakuwa
rahisi kufikia uamuzi wa pamoja.
“Tulifanya mashauriano
yaliyoambatana na hali ya kitafiti na tukaridhika pasipo shaka kwamba
ujio wa Lowassa na wenzake katika chama hiki ni mpango wa Mungu ambao
tunatakiwa tuunge mkono, utusadie kuwaunganisha wenzetu wa CUF, NLD na
NCCR-Mageuzi na Watanzania wote kufikia malengo ya pamoja,” alisema.
“Katika hatua zote hizo tulikuwa sambamba na Dk Slaa lakini katika dakika za mwisho akatofautina kidogo na Kamati Kuu.”
Maelezo
hayo ya Mbowe yanamaliza sintofahamu iliyokuwa imetanda kwa makada wa
Chadema juu ya sababu za Dk Slaa kutoonekana kwenye hafla ya kumpokea
Lowassa Julai 28, wakati wa kuchukua fomu za kugombea urais Julai 30,
siku aliporudisha fomu Agosti Mosi na kwenye vikao vya Sekretarieti na
Kamati Kuu juzi.
Mbowe ambaye pia ni Kiongoni wa
Upinzani Bungeni alisema: “Kwa hiyo tumekubaliana na Katibu Mkuu
apumzike kwa muda na nina hakika kwa tabia na hulka za Dk Slaa… kwa
sababu anajua tunampenda na yeye anakipenda chama hiki, tunamwombea kwa
Mungu ampe nguvu na ujasiri wa kuona kwamba kauli ya wengi ni kauli ya
Mungu.
“Tutaendelea kuongea naye, bado nafasi yake ipo
na kwa wengine wote wenye hofu ya aina hii na naomba niseme kuwa nafasi
zetu za kiuongozi au kiuchaguzi ni dhamana, hakuna yeyote mwenye
hatimiliki na nafasi mliyonayo ni kwa sababu ya watu, tukielewa hivyo
wala hatuna ugomvi.”
Huku akizungumza kwa hisia, Mbowe
alisema kauli yake ni uamuzi wa vikao vya chama na kwamba hakuna ugomvi
wowote na kiongozi huyo, hivyo makada na Watanzania waachane na uzushi
wa mitandaoni akisema hofu kama ya Dk Slaa ipo pia kwa makada wengine na
kwamba ilikuwa na mashiko na inayozungumzika, lakini wasingezuia
matakwa safari ya mamilioni kwa “sababu ya matakwa ya Mbowe au Slaa...
tunasema lazima tuendelee kwa sababu uchaguzi upo kesho.”
Katika
hotuba hiyo ya dakika 35, Mbowe alisema Dk Slaa ni kiongozi ambaye
wanamheshimu, wanampenda na wataendelea kumpenda siku zote kwa sababu
chama chao ni cha kujengana na siyo kubomoana.
Ili
kupitisha uamuzi huo, Mbowe aliwahoji wajumbe wa baraza hilo iwapo
wanataka waendelee na kazi au wasubiri ili kila mmoja afanye uamuzi wake
binafsi na kujibiwa “tuendelee…”
Aliuliza swali hilo
mara mbili na kuungwa mkono na wajumbe wote kwa sauti kubwa na
alipowataka wajumbe wanaounga mkono uamuzi huo wasimame, walifanya hivyo
na kuimba wimbo wa chama “Chadema, Chadema…people’s power.”
Alisema
amezungumza suala hilo mbele ya wanahabari ili kama kuhukumiwa,
ahukumiwe kwa sababu wajibu wake akiwa kiongozi ni kusema ukweli daima.
Aliwataka makada wa Chadema wawe na amani na kwamba chama hicho kipo salama na wanaofikiri kitameguka ni ndoto za mchana.
“Wengine
wakasema Lissu (Tundu) huyoo, wakahamia Mnyika (John), Mnyika alikuwa
mgonjwa, huyoo… mtasema na Slaa amesharudisha na gari mtakuta Jumatatu
huyooo, lakini kwa leo amepumzika mzee wangu,” alisema Mbowe na
kushangiliwa.
Mwenyekiti huyo aligusia moja ya ajenda
ya mkutano wa Baraza Kuu kuwa ilikuwa ni kujadili ilani ya uchaguzi
kabla ya kupitishwa leo na mkutano mkuu.
Baada ya
mkutano huo, kuanzia kesho kwa siku tatu mfululizo chama hicho kitakuwa
na vikao vya Kamati Kuu kuteua majina ya wabunge na wawakilishi
watakaosimamishwa na chama hicho.
Hofu ya Lowassa
Akizungumzia
hofu iliyotanda baada ya Lowassa kujiunga na chama hicho, Mbowe alisema
kila jambo jema mara nyingi hujitokeza likiwa na changamoto.
Alisema
baada ya kutambulishwa kwa Lowassa, hofu ilionekana kutanda ndani ya
wajumbe wa Mkutano Mkuu na Baraza Kuu kwa kuhofia nafasi za uongozi na
hatima ya chama hicho.
“Lakini inawezekana hofu hiyo
wameipata zaidi CCM, kwa kipigo ambacho wamekipata hakijawahi kutokea
katika historia ya siasa nchini, hali hii inataka kufanana na kuondoka
kwa Augustino Mrema lakini naweza kuilinganisha nguvu ile kwa asilimia
25 tu na nafasi ya kuondoka Lowassa.”
Kuhusu madai ya
kupokea mafisadi ndani ya chama, Mbowe alisema katika mazingira yoyote
kwa mwanasiasa anayetafuta mbadala wa chama, lazima atakifikiria Chadema
kwa sababu ni chama kilichojijengea msingi.
Alisema ilikuwa ni lazima kwa chama kuweka mkakati wa kumpokea mwanasiasa yeyote atakayekuwa tayari kuingia.
“Kwa
mpango huohuo wa Mungu, leo yamejitokeza makundi yameingia ndani ya
chama na miongoni mwao aliyekuwa anawika sana ni Lowassa... sasa katika
siasa kuna kitu kinaitwa ‘game change’, yaani kwamba siasa zinaelekea
mrengo huu halafu ghafla zinageuka na kuelekea mrengo mwingine, hiyo
ndiyo ‘dynamism’ ya siasa.
“Hatuwezi kufunga milango ya
chama kwa kuhofia nafasi zetu za uongozi, eti nafasi ya mwenyekiti,
udiwani itachukuliwa...je, tutakuwa tunajenga chama?
“Hali
hiyo ndiyo imekuwa sababu vyama vingi vilijisahau na kuendekeza
masilahi binafsi wakasahau masilahi mapana ya chama. Kila mwanachama
anaheshimika katika nafasi yake ndani ya chama. Kwa hivyo fursa
iliyojitokeza usipoitumia utakuwa ni mwendawazimu.”
Mwalimu abeba mikoba ya Dk Slaa
Chama
hicho kimemkaimisha Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu nafasi ya
Dk Slaa na papo hapo, Mwalimu aliwaeleza wajumbe kuwa hotuba maalumu ya
Katibu Mkuu itatolewa leo wakati wa mkutano mkuu.
“Lazima
mjue tunakwenda kuwa chama tawala, hivyo hakuna kiongozi mdogo wala
hakuna mwanachama aliye mdogo ndani ya chama hiki, kila mwanachama mmoja
atakuwa na thamani, hivyo mjilinde msije kunufaisha maadui zetu,”
alisema Mwalimu.
Msindai atua Chadema
Mwenyekiti
wa wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai jana alijiunga na Chadema na
kutambulishwa katika mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho.
Mgana,
ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Iramba Mashariki (2000-2010)
alitambulishwa pamoja na Mbunge wa Arumeru Magharibi (CCM), Goodluck Ole
Medeye na ofisa mwandamizi wa chama hicho, Matson Chizii.
Makada
hao wa CCM jana usiku waliambatana katika kikao hicho na aliyewahi kuwa
waziri mkuu Edward Lowassa. Habari zinasema kuna makada zaidi wa CCM
wakaotambulisha katika mkutano mkuu wa Chadema leo.
Chadema yamweka pembeni Dk Slaa
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 04, 2015
Rating:
No comments:
Post a Comment