MFUKO wa Umoja wa Mataifa
wa Ukuzaji Mitaji (UNCDF) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), umeitisha kongamano la siku mbili la
upatikanaji wa fedha za ndani kwa maendeleo.
Kongamano hilo
linahusisha wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa nchini Tanzania na linashirikisha
watu 110.Pamoja na wakurugenzi hao, wapo na wawakilishi kutoka Serikali Kuu na wawakilishi
walioteuliwa kutoka serikali za mitaa za Uganda, Senegal na Benin.
Kwa mujibu wa taarifa ya
UNCDF, nia ya kongamano hilo ni kuonesha mafanikio ya mfumo wa ukusanyaji wa
fedha za ndani kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi ya kibiashara katika
nchi za Tanzania na Uganda.
Taarifa hiyo imesema
kwamba baada ya kujifunza mafanikio hayo washiriki watajadiliana na kujipanga
kwa ajili ya utekelezaji wa mfumo huo katika nchi zao wanaokotoka ili kupiga
hatua mbele katika uendelezaji wa miradi bila kutegemea fedha za nje.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi Katibu Mkuu Tamisemi, Jumanne Sagini alisifu kazi inayofanywana
programu ya uwezeshaji wa fedha za ndani kwa maendeleo ( Local Finance
Initiative- LFI) chiniya sekretarieti ya UNCDF kwa ubunifu wake unaowezesha kupatikana
kwa mitaji ya kuwekeza katika miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na serikali za
mitaa.
Aidha alielezea dhamira
ya serikali ya kutumia mfumo huo ulioasisiwa na UNCDF kwa kuufanya uwe wa
kitaasisi zaidi ili kuweza kusaidia kutekeleza mipango ya maendeleo na
uwekezaji ya serikali za mitaa.
Akizungumzia umuhimu wa kongamano hilo, Mgeni rasmi, Mratibu wa
Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Alvaro Rodriguez, aliipongeza serikali ya
Tanzania kwa kufuata mfumo wa utafutaji wa fedha za ndani kwa ajili ya kukuza
uwekezaji katika miundombinu ya kibiashara inayoleta mabadiliko kwa umma.
Rodriguez alisema katika hotuba yake kwamba kwa kuwezesha mfumo
wa UNCDF kwenye serikali za mitaa ndio jibu la uhakika la uwekezaji wenye
mafanikio endelevu kwa taifa zima.
Aidha alisema mpango huo wa LFI ambao umekuwepo nchini kwa miaka
mitatu na kuwezesha kuleta mabadiliko katika jamii, unafaa kumilikiwa na jamii
ili kuwezesha mafanikio ya juu katika uwekezaji.
Mratibu huyo alisema kwamba Umoja wa Mataifa kupitia UNCDF
utaendelea kufanyakazi na serikali ya Tanzania,kwa kuwa wanaamini kwamba vita
dhidi ya umaskini itafanikiwa kwa kuhamisha mitaji na kuipeleka katika ngazi za
chini kwa maendeleo ya wananchi.
Kongamano hilo ambalo ni mwendelezo wa uwezeshaji na
kubadilishana uzoefu na elimu kwa lengo la kuwezesha miradi ya umma na binafsi
inayochagiza maendeleo kujengwa; katika siku ya kwanza ya kongamano hilo
washiriki wataoneshwa miradi iliyotekelezwa manispaa ya Busia Uganda na Kibaha
nchini Tanzania.
Manispaa ya Busia
imejenga kituo cha malori, ushuru wa forodha na maeneo ya kufanyia biashara,wakati
Kibaha wamejenga kituo cha kisasa cha mabasi na soko.
Timu ya wataalamu wa UNCDF watawafundisha washiriki kwa siku 2
kuhusu miradi ya maendeleo, awamu za malipo ya fedha na mikakati ya kupata
fedha na malipo na mbinu za kupunguza hatari za kibiashara.
Akisisitiza umuhimu wa kongamano hilo Mkuu wa UNCDF nchini na
Meneja wa LFI duniani Peter Malika alisema kwamba kongamano hilo linatoa nafasi
kwa watumishi wa serikali za mitaa na wengine kujifunza namna mpya ya kupata
mitaji kwa kutumia vyanzo vya nyumbani ili kufadhili miradi ya miundombinu ya
kiuchumi inayohitajika kwa ajili ya kutoa fursa za ujasiriamali , biashara,
uwezeshaji, ajira, kuboresha maisha ya watu, ukusanyaji kodi na utoaji huduma.
Kongamano hilo la siku 2 ni miongoni mwa juhudi kadha za UNCDF
za kuwezesha serikali za mitaa kufikia maendeleo endelevu na kuleta athari
chanya kwa jamii ili kuondoa umaskini.
KONGAMANO LA UPATIKANAJI WA FEDHA ZA NDANI ZA MAENDELEO LAFANYIKA JIJINI ARUSHA
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 06, 2015
Rating:
No comments:
Post a Comment