Ripoti ya tume ya kuhakiki mali za CCM
iliyoundwa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli imebaini uwepo wa
upotevu mkubwa wa mali za chama uliosababishwa na mikataba mibaya, ubadhirifu,
wizi, usimamizi mbaya wa mali, utapeli na ukosefu wa maalidili katika
uendeshaji wa miradi ya chama
Baada ya Rais Magufuli kupokea ripoti ya
tume hiyo iliyoongozwa na Dk Bashiru Ally, alisema itapelekwa katika kamati kuu
na halmashauri kuu ndani ya mwezi huu ili kuijadili na viongozi kutoa maelekezo
“Huwezi ukaanza kupiga vita rushwa na ufisadi
ndani ya Serikali wakati chama kina rushwa na ufisadi, chama nacho tunataka
tukisafishe, mambo ya rushwa na ufisadi yaishe ili Tanzania iende vizuri, ndio
maana tumeunda tume ya Dk Bashiru Ally, imefanya kazi nzuri sana na ripoti hii
tutaipeleka kamati kuu na halmashauri kuu ndani ya mwezi huu ili tuijadili na
viongozi watoe maelekezo.”
Rais Magufuli aliwaagiza wajumbe wa
sekretarieti ya CCM waliohudhuria hafla ya uwasilishwaji wa ripoti hiyo kuanza
kufanyia kazi baadhi ya mambo yaliyo ndani ya uwezo wao na kwamba masuala
mengine yataamuliwa na vikao vya juu vya chama
Akizungumzia changamoto ilizokabiliana nazo,
Rais Magufuli alisema, “Nilipokuwa nateua tume hii nilikuwa najua ugumu wa
kazi, nilikuwa najua kuwa mtapata shida kwenda kuwahoji watu licha ya kwamba
niliwapa uhuru wa kumhoji mtu yeyote na mmefanya kazi nzuri sana, kilichobaki
sasa ni kuifanyia kazi.”
Awali, Dk Bashiru alisema uhakiki huo
umefanywa kwa mali za chama hicho tawala zilizo chini ya baraza kuu, jumuiya za
chama na kampuni zake
Alisema wakati wa utekelezaji wa kazi hiyo,
walitembelea maeneo yenye mali za chama hicho, kuwahoji watu mbalimbali
wakiwamo viongozi waliohusishwa na mali zilizokuwa zikihakikiwa
Alisema kamati imepitia nyaraka na
kufuatilia uhalisia katika ofisi za mamlaka husika, kufanya uchambuzi wa
taarifa na kutoa mapendekezo
Akizungumzia ripoti hiyo, Makamu Mwenyekiti
wa CCM Phillip Mangula aliipongeza tume hiyo kwa kazi kubwa iliyoifanya na
kusisitiza taarifa yake imedhihirisha kuwa baadhi ya watu waliooneka kukisaidia
chama hawakuwa wanakisaidia, bali walijinufaisha
Tume hiyo ilitangazwa Desemba 20, mwaka jana
ikiwa na wajumbe tisa. mbali ya Dk Bashiru, wengine ni Walter Msigwa, Albert
Msando, Galala Wabanhu (Hananasif), Albert Chalamila, William Sarakikya,
Komanya Kitwara, Dk Fenela Mkangara na Mariam Mungula.
Ripoti mali za CCM yabaini wizi, utapeli
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 22, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 22, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment