Mkurugenzi wa Kampuni
ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40), maarufu Dk Manguruwe na
Mkaguzi wa kampuni hiyo, Rweyemamu John (59) wamefikishwa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka 28 yakiwemo ya kuendesha
biashara ya upatu na utakatishaji fedha kinyume cha sheria.
Inadaiwa
washtakiwa hao walijipatia Sh92.2 milioni kutoka kwa watu 19 tofauti, ambao
walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa kuwaahidi kuwa watapata faida mara mbili
hadi tatu ya fedha walizotoa.
Washtakiwa
hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Jumanne, Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi
ya uhujumu uchumi namba 31523 ya mwaka 2024 na Wakili wa Serikali Mwandamizi,
Job Mrema mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya.
Hata
hivyo, kabla kusomewa mashitaka hayo, Hakimu Lyamuya aliwaambia washtakiwa hao
hawaruhusiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza
kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.
Pia,
mashitaka yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo wataendelea
kubaki rumande.
Kati
ya mashitaka hayo 28, 19 ni ya kuendesha biashara ya upatu na tisa ni ya
utakatishaji.
Katika
moja ya mashitaka ya kuendesha biashara ya upatu, washtakiwa wanadaiwa
kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi,2023, jijini Dar es Salaam,
walitenda makosa hayo.
Inadaiwa
kuwa Mkondya akiwa kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo na John akiwa Mkaguzi wake
waliendesha biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu watapata pesa mara mbili hadi
tatu kama faida zaidi ya waliyotoa.
Inadaiwa
washtakiwa hao walijipatia Sh92.2 milioni kutoka kwa watu 19 tofauti ambao
walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa kuwaahidi kuwa watapata faida mara mbili
hadi tatu ya fedha walizotoa.
Katika
mashitaka 19 ambayo ni ya utakatishaji yanayomkabili Mkondya peke yake,
inadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 akiwa katika
Mkoa wa Dar es salaam na akiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni hiyo alijipatia jumla
ya viwanja tisa katika kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe.
Inadaiwa
kuwa mshtakiwa huyo alijipatia viwanja hivyo huku akijua ni mazalia ya
makosa tangulizi ya kiendesha biashara ya upatu.
Baada
ya kusomewa mashitaka hayo, upande wa mashitaka umedai kuwa upelelezi wa shauri
hilo bado haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu
aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 19, 2024 kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa
wote amerudishwa rumande kutokana na mashitaka yanayowakabili hayana dhamana
kwa mujibu wa sheria.
No comments:
Post a Comment