VILIO VYA MAWAKALA KILA KONA BAADA YA TOZO MPYA

 
Wakati wananchi wakilazimika kutafuta njia mpya isiyo na gharama kubwa kutuma na kutoa fedha, mawakala wa huduma za fedha kupitia simu za mkononi wamelalamika kukosa wateja, hivyo kuathirika kimapato.

Malalamiko ya mawakala hao yametolewa siku mbili tangu kuanza kutekelezwa kwa kodi ya uzalendo iliyoongeza gharama ya kutuma au kutoa fedha kwa simu ya mkononi kwa kati ya Sh10 mpaka Sh10,000.

Mawakala hao wanasema wateja walianza kupungua Julai 15 kodi hiyo ilipoanza na kadri siku zinavyokwenda ndivyo wanavyozidi kupungua.

Wanasema wateja waliokuwa wanafanya miamala kwa siku wamepungua kwa zaidi ya robo tatu.

Josiah Lairumbe, wakala anayetoa huduma Soko Kuu jijini Arusha, alisema mbali ya idadi ya wateja kupungua kuanzia juzi, pia malipo ya bidhaa kielektroniki kupitia simu za mkononi nayo yameshuka.

“Tuzilijua taarifa za ongezeko la gharama za kutuma na kupokea fedha lakini hatukutarajia viwango vikubwa kiasi hiki. Siku ya kwanza tu nimepoteza wateja wawili wakubwa waliokuwa wananunua bidhaa na kulipa kwa simu,” alisema Lairumbe.

Akionyesha kukata tamaa, wakala huyo aliiomba Serikali kurejea upya viwango hivyo kwa sababu vitasababisha madhara si kwa mawakala pekee, bali wananchi wenye kipato cha chini, hasa wa vijijini ambako hakuna huduma za benki.

Wakala mwingine sokoni hapo, Mary Kileo alisema tangu juzi hadi jana mchana aliwahudumia wateja watano, tofauti na zamani idadi hiyo ilikuwa inazidi wateja 100 kwa siku.

Mjini Moshi, Cosma Shirima alisema tozo mpya zitaathiri ajira za vijana wengi wanaofanya uwakala. “Wateja wamepungua tangu viwango vipya vilipoanza, sijui maisha yatakuwaje hali hii ikiendelea kwa sababu ndio kazi inayoendesha maisha yangu. Sijui nitafanya nini nitakapolazimika kufunga biashara kwa kukosa wateja,” alisema.

Hofu ya kukosa ajira pia ilionyeshwa na Asia Mustapha, wakala aliyepo eneo la Mnara wa Samaki jijini Mwanza. “Hali ikiendelea hivi ni dhahiri tutafilisika na kufunga biashara. Serikali itaingiza fedha kupitia tozo hizi, lakini itapunguza ajira badala ya kuziongeza. Hii itakwamisha lengo la kutengeneza ajira mpya,” alisema Asia.

Huduma za fedha kwenye simu za mkononi zilianza kutolewa nchini zaidi ya muongo mmoja uliopita na mpaka sasa kuna zaidi ya watumiaji milioni 32 wanaohudumiwa na Mpesa, Tigopesa, Airtel Money, Halopesa, Easypesa na TTCL Pesa kupitia mawakala zaidi ya 300,000 waliosambaa kote nchini.

Mawakala wengi ni vijana, wakiwamo wahitimu wa vyuo vikuu ambao baada ya kukidhi vigezo vya kurasimisha biashara zao huruhusiwa kutoa huduma hizo.

Tanzania inakadiriwa kuwa na wahitimu zaidi ya 800,000 kila mwaka, lakini ni chini ya asilimia 10 wanaopata ajira kwenye soko rasmi.

Baada ya muda mrefu wa kuwahudumia wananchi, kundi hilo sasa linapata changamoto inayohusisha kupungua kwa wateja hivyo kushusha kamisheni wanayoipata.

Uzoefu nje ya Tanzania

Tanzania sio nchi ya kwanza kutoza kodi hii ya miamala ya simu. Mataifa mengi yaliyoendelea yanafanya hivyo ili kutekeleza miradi waliyoikusudia.

Mhadhiri wa kodi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), CPA David Mwakapala alisema nchi za Scandinavia zinaongoza kwa kodi hata sasa, Sweden imeanzisha kodi ya miamala ya simu.

Hata hivyo, alisema kuna tofauti kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea, ikiwamo Tanzania zinazotokana na utamaduni.

“Wanatuzidi kwenye kutoa taarifa kwa wananchi na kuwaonyesha umuhimu wa kodi husika. Kule wananchi wengi wanakuwa wanafahamu kabla kodi haijaanza kutozwa, lakini hapa kwetu, watu walianza kujua walipopokea ujumbe kutoka kampuni za simu ndio maana panic (hofu) ilikuwa kubwa,” alisema Mwakapala.

Mataifa kadhaa Afrika ikiwamo Uganda, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Ivory Coast yaliwahi kuanzisha kodi hiyo, lakini malalamiko ya wananchi yalizilazimu Serikali ama kuifuta au kupunguza kiwango kilichopendekezwa.

Kwenye bajeti yake ya mwaka 2019/20, Malawi ilianzisha kodi ya zuio ya asilimia moja kwenye kila muamala unaofanywa, lakini hoja zilizotolewa na Shirikisho la Mabaraza ya Kutetea Wateja (Cama), watoa huduma wenyewe na wananchi yalimlazimisha Waziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo nchini humo, Joseph Mwanamvekha kubatilisha kodi hiyo.

Mpaka Juni 2019 wakati kodi hiyo inapitishwa, Malawi ilikuwa na wateja milioni saba waliosajiliwa, huku asilimia 37.4 tu kati yao wakitumia huduma za fedha. Hata Uganda iliyopitisha kodi ya asilimia moja kwenye kila muamala wa kutuma au kutoa fedha na kulipia huduma au bidhaa na kutoza Sh200 za Uganda kwa kila mtumiaji anayeingia Facebook, WhatsApp na Skype, ililazimika kuipunguza.

Waziri wa Mipango nchini humo, David Bahati aliisitisha akisema “ilipitishwa kimakosa.”

Kwenye ripoti yake iliyochapishwa na Taasisi ya Brookings ya Marekani inayoitwa “Taxing mobile phone transactions in Africa: Lessons from Kenya,” gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Kenya, Njuguna Ndung’u anasema “mchango wa kodi ya miamala ni asilimia moja tu kwenye pato la Kenya. Ni mdogo. Hili ndilo jambo muhimu kuzingatia, sio kwa Kenya pekee bali mataifa yote yenye nia ya kuongeza kodi ya miamala.”


Biashara mtandaoni

Ukiacha mawakala, wengine ambao kipato chao wanasema kimeshuka ni wanaofanya biashara mtandaoni wakitegemea malipo yanayofanywa kielektroniki kupitia simu ya mkononi.

Muuzaji wa saa na urembo jijini Dar es Salaam, Zainabu Ally alisema huenda biashara yake ikatetereka kutokana na wateja kushindwa kumudu gharama za kutuma fedha, naye kutoa kwa sababu kunaongeza gharama.

“Mwanzoni nilikuwa nawaambia wateja wanitumie kwenye simu, baada ya kuona faida yangu inaathirika nikajisajili kama wakala wa mitandao karibu yote, mtu akitaka kunitumia fedha namwambia atoe ili nipate pesa taslimu, lakini sasa gharama ya kutoa imekuwa mzigo kwao,” alisema.

Tangu kodi mpya ilipoanza kwenye miamala, alisema wateja wake wanamuuliza kama ana akaunti ya benki ili wamuingizie fedha huko badala ya kutoa kwa wakala.

Mfanyabiashara Moreen Kiya, ambaye humpelekea mteja bidhaa aliyoichagua mahali alipo baada ya kuichagua kwenye akaunti za mitandao yake ya kijamii, alisema tangu juzi hajapokea oda yoyote.

VILIO VYA MAWAKALA KILA KONA BAADA YA TOZO MPYA VILIO VYA MAWAKALA KILA KONA BAADA YA TOZO MPYA Reviewed by KUSAGANEWS on July 18, 2021 Rating: 5

No comments: