Kwa Kipindi cha Miaka Miwili na Nusu Shule 5 za Msingi zimengwa na za Sekondari 3 Ngorongoro

Mbunge wa jimbo la Ngorongoro ambaye pia ni naibu waziri wa Elimu sayansi na Teknoloji Mh William Olenasha amesema tangu apewe dhamana ya kuongoza wanachi wa Ngorongoro amehakikisha elimu inaboreshwa na watoto wanaenda Shule.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika muendelezo wa ziara yake ya kutembelea wananchi wake ili kuwaeleza mafanikio aliyoyapata kwa kipindi cha miaka miwili na nusu katika kata ya Malambo Olenasha amesema mpaka sasa tangu achaguliwe kumejengwa shule tano za msingi na Shule tatu za Sekondari.

Mh Olenasha amesema kuwa kwasasa kila mtoto anatakiwa kwenda shule kwasababu elimu ndiyo msingi wa maisha ya baadae hivyo wazazi wanatakiwa kuhamasisha watoto wao wasikose masomo.

Amesema kwa kupitia ilani ya chama cha mapinduzi ambayo inatekelezwa na serikali ya awamu ya tano kupitia Raisi Dokta John Magufuli inahakikisha kila mtoto anapata elimu kwasababu imewapunguzia wazazi mzigo kutokana na elimu bila Malipo.

Naye Diwani wa kata ya Malambo kupitia Chadema Bwana Abraham Labi amesema kuwa anachokifanya Mbunge Olenasha ni cha kupongezwa kwasababu hana ubaguzi na hachagui maeneo ya kupeleka maendeleo anafanya haki kwa kila mwanachi wa Ngorongoro hivyo anastahili Pongezi.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake wilayani Ngorongoro Nalepo Emanuel amesema kuwa wanampongeza Mbunge wao Olenasha kwasababu ametengeneza miundombinu ya Elimu ambapo licha ya kuwepo shule mpya pia shule za zamani zimeongezewa madarasa mapya.

Amesema mwanzo wanafunzi walikuwa wanatembea umbali mrefu kwenda kufuata shule ambapo kipindi cha mvua walikuwa hawawezi kwenda kutokana na kushindwa kuvuka mito ambayo inajaa maji.

Ameongeza kuwa tangu Olenasha amechaguliwa wilaya ya Ngorongoro imefahamika kwa kuwa na maendeleo zaidi ambayo yamekuja kwa kasi kuliko vipindi vingine vilivyopita.

Akizungumza mmoja wa mwanafunzi ambaye anasoma Shule ya Msingi Malambo John Lengai amesema kuwa mwanzo kabla ya kuwepo shule hiyo alikuwa anatembea umbali wa kilomita kumi hivyo wakati mwingine kushindwa kuhudhuria shule kutokana na changamoto za mvua pamoja na umbali huo.

Baba Lapoi Ndesi ambaye ni mzazi amesema kuwa elimu imeboreshwa hata watoto wanahamasika kutokana na shule kuwa karibu na imepunguza kitendo cha watoto wengine kukataa kwenda shule kutokana na kusingizia umbali.

Amesema kama wazazi walikuwa wanalazimika kusindikikiza watoto shule kutokana na wengine kuwa wadogo ivyo kushindwa kufanya shughuli za maendeleo na muda mwingi kupoteza barabarani lakini kwasasa wanamshukuru Mbunge wao kwa kuendelea kuboresha elimu.



Kwa Kipindi cha Miaka Miwili na Nusu Shule 5 za Msingi zimengwa na za Sekondari 3 Ngorongoro Kwa Kipindi cha Miaka Miwili na Nusu Shule 5 za Msingi zimengwa na za Sekondari 3 Ngorongoro Reviewed by KUSAGANEWS on July 13, 2018 Rating: 5

No comments: