Wakati watu wakisubiri kuona spidi
ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Mh. Kangi Lugola itakapokwamia, kiongozi huyo
ameonesha kutotabirika kutokana na vitendo vyake vinavyotokea kila siku ndani
ya utendaji wake wa kazi.
Spidi
ya Waziri Lugola, inazidi kwenda mbele zaidi, baada ya tukio la leo la
kumwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kumuweka rumande Askari Polisi
aliyeshindwa kujibu swali lake lililohoji, "ni vitabu gani muhimu vinastahili
kuwekwa katika kituo cha polisi kwa ajili ya kutoa msaada wa huduma kwa
raia"?
Lugola
ametoa agizo hilo leo alipokuwa Arusha katika ziara yake ya kikazi ambayo
ilikuwa ikihusisha kukutana na wadau wa utalii pamoja na kujadili mambo ya
usalama na ajira kwenye sekta hiyo.
Hata
hivyo baada ya agizo lake kuchukuliwa hatua Waziri Lugola alimtaka RPC kumtoa
rumande askari huyo kwa kuwa amegundua kwamba askari huyo anakosa uelewa wa
masuala ya utalii pamoja na diplomasia.
Tukio
la Waziri Lugola la kumuweka na kumtoa rumande askari polisi linakuja
ikiwa siku chache tuu kupita tangu kutoa tamko la kutafutwa kwa mbwa kisha
kusitisha tamko hili na kuzuia jamii ya kitanzania hususani waandishi wa
habari kuacha kufuatilia tukio la kupotea mbwa wa Jeshi la Polisi anayejulikana
kwa jina la Hobby, kwa kuwa jambo hilo kwa sasa lipo chini ya uchunguzi.
Julai
19, 2018, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alibaini upotevu wa mbwa huyo
wakati alipokuwa kwenye ziara yake katika Kikosi cha Farasi na Mbwa kilichopo
eneo la Bandari Jijini Dar es Salaam na kumuagiza IGP Sirro kutoa maelezo ya
upotevu wa mbwa.
Pamoja
na hayo, Waziri Lugola ameshamtaka IGP Simon Sirro amtafute mmiliki wa kampuni
ya Lugumi popote pale alipo na kumfikisha ofisini kwake Julai 31 saa mbili
asubuhi ili ajue hatma yake ikiwa ile ya kudaiwa kuwepo na ufisadi.
Sakata
la Lugumi liliibuka bungeni kwa kile kilichodaiwa kuwa zipo dalili za ufisadi,
kutokana na Sh. bilioni 34 zilizolipwa kwa kampuni ya Lugumi iliyopewa tenda ya
kufunga vifaa vya kielektroniki vya kutambua alama za vidole kwenye vituo vya
polisi nchini ambapo mpaka sasa zoezi hilo limeshindwa kukamilishwa..
Mbali
na hilo Waziri Lugola pia amemuagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa (NIDA) afike ofisini kwake Julai 25 akiwa na waliopewa tenda ya kuleta
mtambo wa kutengeneza vitambulisho vya taifa ili kwenda kumueleza kwani mtambo
huo haujaletwa au waende na pesa walizopewa na Serikali.
Waziri
Lugola tayari ameshatoa matamko mengi na sasa ikiwa ni wiki ya tatu tangu
alipoapishwa, kwa mujibu wake amesema anajitahidi kufanyia kazi maagizo yote
aliyopatiwa wakati anaapishwa na kama Waziri ni wajibu wake kutafuta matokeo
chanya ya haraka ili Rais aweze kupumzika na kuwatumikia wananchi kwenye
maendeleo
Kasi ya Kangi haina kikomo na haitabiriki.
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 23, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment