Wananchi wa kijiji na Wilaya
ya Mvomero mkoani Morogoro, wamehoji juu ya shamba lenye ekari 326 lililofutiwa
hatimiliki na Rais, kurudi kwa mmiliki wa awali.
Walisema wanashangazwa kuona shamba
hilo lililokuwa likimilikiwa na Esther Sumaye – mke wa Waziri Mkuu mstaafu
Fredrick Sumaye, likiendelezwa kwa kilimo, kuchimbwa visiki na kukodishwa kwa
wananchi, huku viongozi wakiwa kimya bila kutoa taarifa yoyote ya mabadiliko ya
umiliki wake.
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa
Kitongoji cha Kijoja, Ally Saleh, alisema wameshtushwa na taarifa iliyotolewa
na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mohamed Utali kuwa shamba hilo limerudi kwa
mmiliki wake wa mwanzo, Esther kutokana na uamuzi uliotolewa na mahakama baada
ya kukata rufaa na kushinda kwa mujibu wa sheria.
“Tunashangaa kusikia kwamba eti
shamba ambalo liko katikati ya kijiji na lilirudishwa kwa wananchi na Rais,
barua tulipewa, lakini kwa sasa tunaambiwa kijuujuu tu kuwa limerudi kwa Esther
Sumaye bila uthibitisho wowote,” alisema Saleh.
Nao wananchi wa kijiji hicho, Said
Ally, Said Kibeku na Maila Suteli, walisema wanalitegemea eneo la shamba hilo
kwa maendeleo ya kijiji, ikiwamo ujenzi wa makazi, viwanda, shule na zahanati
kutokana na kuchukua eneo kubwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya
Mvomero, Utali, alisema halmashauri ilikuwa katika harakati za kutaka kuligawa
shamba hilo kwa wananchi kama maelekezo ya Serikali yalivyotaka, lakini
ilishindikana baada ya kupokea barua ya kuwa shamba limerudi kwa Esther.
“Tulipokea barua iliyoambatana na
hukumu kutoka kwa mwanasheria wa Esther Sumaye kuwa mahakama imempa ushindi
Esther Sumaye katika kesi namba 25 ya mwaka 2016, hivyo hatuwezi kukurupuka na
kuingilia eneo ambalo lina hukumu ya mahakama,” alisema Utali.
Wananchi Waiomba Serikali Iwagawie Shamba La Sumaye
Reviewed by KUSAGANEWS
on
June 01, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment