SHIRIKA LA UNESCO LAWA MSAADA KWA JAMII YA KIFUGAJI ILI KUACHANA NA UKEKETAJI KWA MTOTO WA KIKE


Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO)  linaratibu kampeni ya mwezi mmoja ili kupambana na ukeketaji kwa mtoto wa kike katika mikoa mitano inayoongoza ikiwemo mkoa wa Manyara, Dodoma, Arusha, Mara na Singida. 

Kampeni hiyo imeandaliwa kwa msaada wa kifedha kutoka kwa mradi wa SDC, Mradi wa Sida O3 na UNDAP II- VAWC na Mfuko mmoja wa Umoja wa Mataifa.

Kampeni hiyo ambayo imeanza wilayani Ngorongoro Mei 28  inajumuisha warsha ya siku 3 ya kujenga uwezo kwa kufanya kazi kwa kushirikiana na radio ya kijamii ya Loliondo FM inayofadhiliwa na  UNESCO.

Warsha hiyo itafuatiwa  na uzinduzi rasmi wa kampeni  Mei 31 lengo likiwa ni kukomesha ukeketaji mila ambayo imeota mizizi katika wilaya ya ngorongoro.

Warsha hiyo inalenga kuongeza jitihada za kampeni muhimu za kupambana na ukeketaji na  inawashirikisha waandishi wa habari,malaigwanani,viongozi wa dini,mangariba na watendaji wa serikali.

Kampeni kupitia redio jamii inatarajiwa  kuwafikia watu milioni 1.

Radio jamii zinazoshiriki  kwenye kampeni hiyo na mikoa yake kwenye mabano ni Loliondo FM (Arusha), ORS (Manyara), Dodoma FM (Dodoma)Triple A FM (Arusha), na Mazingira FM (Mara).

Mpango mkakati wa kampeni hiyo ni kupambana na ukeketaji wilayani Ngorongoro pamoja kwa kupitia Kampeni kwa Umma kwa njia ya Radio za jamii ambapo radio zitatengeneza vipindi  na kuwashirikisha viongozi wa jamii, wasaidizi wa sheria, wafanyakazi wa afya, viongozi wa kidini, Ngariba na vijana (wasichana walioko mashuleni na wale walioko nje ili kuunganisha nguvu kupinga ukeketaji.

Njia nyingine itahusisha kampeni  mashuleni, huku ikiwalenga wanafunzi, walimu, na kamati za wazazi wa shule katika shule 20  zilizoko katika eneo la wilaya hiyo.

Wakati huo huo, kampeni ya jamii itafanyika hasa kwa wazazi na walezi katika vijiji 14 ambavyo vitafanya mikutano kijiji kwa kijiji kwa ajili ya uhamasishaji.

Kampeni hiyo inafanyika mwezi Juni kutokana na kipindi cha mwezi huo kukithiri kwa vitendo vya ukeketaji  ambapo wazazi hutumia fursa ya watoto wa kike kuwa likizo na hivyo kuwakeketa. 


 Kampeni hii imeandaliwa na UNESCO  kwa Ushirikiano wa karibu na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Baraza la Viongozi wa Jadi  na Mila wa Kimasaai na Mtandao wa Redio za Jamii  Tanzania (TADIO).

Kupitia mkakati wake  wa kijamii na kiutamaduni, kampeni za UNESCO zimepata mwitikio mkubwa kutoka kwa jamii ikiwemo mabadiliko ya fikra kwa baadhi ya viongozi wa jadi na Ngariba (wakeketaji.)

Kampeni ya kupambana na ukeketaji  ni mwendelezo ambapo mnamo  mwezi Juni na  Disemba 2017  kampeni kama hii ilifanyika ambapo wasichana 10 waliokolewa mikononi mwa ngariba kabla hawajakeketwa huku  wawili wakiokolewa na ndoa za utotoni kwa wazee wenye umri wa miaka 68.

Nchini Tanzania, Ukeketaji ni desturi iliyoota mizizi katika mila za baadhi ya makabila  ambapo hutumika kama namna ya kumtoa mtoto wa kike kutoka daraja moja la utoto na kwenda kwenye utu uzima. 


Makabila ambayo yamebobea katika ukeketaji nchini ni Wamasai, Wakurya, Wagogo, Wanyiramba, Wambulu ,Wachagga na  Wapare. Kwa mujibu wa Taarifa ya Utafiti wa  Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania wa mwaka 2015/2016 (TDHS-MIS, 2015-16),  mwanamke mmoja kati ya wanawake kumi nchini Tanzania amekeketwa.

 Mikoa mitano inayoongoza kwa ukeketaji nchiini Tanzania na asilimia katika mabano ni Manyara (58%), Dodoma (47%), Arusha (41%), Mara (32%) na Singida (31%).

Ukeketaji una madhara mengi ya afya ikiwa ni pamoja na maambukizi ya mara kwa mara katika njia ya mkojo na uke, fistula ( kushindwa kuzuia haja ndogo na kubwa), maumivu ya muda mrefu, kuchanika wakati wa uzazi na kuvuja damu nyingi wakati wa uzazi na hata kusababisha kifo. 
Ukeketaji pia una athari za kisaikolojia.

Maswali kwa vyombo vya habari: UNESCO Dar Office, Tanzania | Mathias Herman | +255 755 195 459|m.herman@unesco.org

SHIRIKA LA UNESCO LAWA MSAADA KWA JAMII YA KIFUGAJI ILI KUACHANA NA UKEKETAJI KWA MTOTO WA KIKE SHIRIKA LA UNESCO LAWA  MSAADA KWA JAMII YA KIFUGAJI ILI KUACHANA NA UKEKETAJI KWA MTOTO WA KIKE Reviewed by KUSAGANEWS on May 29, 2018 Rating: 5

No comments: