Na Lilian Lundo – MAELEZO,Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Wanaafrika Mashariki kujiamini kuwa
wanaweza kutekeleza miradi ya maendeleo bila kutegemea mataifa mengine.
Rais Dkt. Magufuli ameyasema hayo
leo Mjini Dodoma alipokuwa akihutubia Bunge la Nne la Jumuiya ya Afrika
Mashariki linalofanyika mkoani humo kwa mara kwanza tangu kuanza kwa
Bunge hilo.
“Ninazungumza hili si kwamba
hatuhitaji msaada au hatuhitaji ushirikiano, lakini ni lazima tuliweke hili
wazi, kwamba tukiamua tunaweza na mifano ipo mingi ikiwemo Tanzania”.
Alisisitiza Mhe. Rais Dkt. Magufuli.
“Tanzania tunajenga reli ya kisasa
yenye urefu wa kilometa 700.26 kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa thamani ya
shilingi Trilioni 7.6, tumeweza kununua ndege sita na pia tumejenga meli kubwa
katika Ziwa Victoria bila kuomba mkopo popote,” amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli ameongeza kuwa
wabunge wa Afrika Mashariki wanaowajibu wa kuhakikisha wanalinda na kuendeleza
mafanikio yaliyopatikana ndani ya Jumuiya hiyo.
Akitaja baadhi ya mafanikio
yaliyopatikana na Jumuiya hiyo Rais Magufuli amesema kuwa kabla ya kuanza kwa
umoja wa forodha mwaka 2005 biashara kati ya nchi wanachama ilikuwa na thamani
ya dola za kimarekani bilioni 1.8 lakini baada ya kuanzishwa kwa umoja wa
forodha imeongezeka hadi kufikia zaidi ya dola za kimarekani bilioni 5.
Mbali na hayo Rais, Magufuli
ameshukuru uamuzi wa bunge hilo kufanyika mjini Dodoma ambapo kwa sasa Serikali
imehamishia shughuli zake zote katika mkoa huo, na tayari watumishi wa serikali
zaidi ya 3000 wameshahamia huku Rais Magufuli akitarajiwa kuhamia muda wowote
mwaka huu.
Kwa upande wake Spika wa Bunge la
Afrika Mashariki Dkt. Martin Ngoga amesema Bunge hilo linasubiri marekebisho ya
mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ili lugha ya Kiswahili ianze
kutumika kama lugha rasmi katika vikao vya bunge hilo na katika jumuiya hiyo
kwa kuzingatia azimio lililokwishapitishwa.
“Hatuoni sababu ya kutumia lugha za
wageni wakati kuna lugha yetu ambayo tunazungumza ambayo ni kiswahili,” alisema
Dkt. Ngoga.
Bunge la Afrika Mashariki
linaendelea na vikao vyake mkoani Dodoma katika ukumbi mdogo wa Bunge wa Pius
Msekwa. Bunge hilo limefanyika kwa mara ya kwanza mkoani humo.
Rais Magufuli; EAC Tunaweza Kujitegemea
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 24, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment