Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni wamesusia kuapishwa kwa wabunge saba Viti Maalumu wa Chama cha Wananchi (CUF) katika mkutano wa nane Bunge la 11 kwa madai hawakufurahishwa na maamuzi ya kufukuzwa wabunge 8 wa Viti Maalumu wa chama hicho.
Mkutano wa nane wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania umeanza leo Mjini Dodoma na moja ya mambo yaliyopo kwenye ratiba ya mkutano huo ni kuapishwa kwa wabunge wapya 8 wa Viti Maalumu ambao wameteuliwa kuziba nafasi za wabunge 8 wa Viti Maalumu waliofutwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba baada ya kupoteza sifa ya kuwa wabunge.
Wabunge ambao wamekula kiapo cha uaminifu siku ya leo Septemba 5 ni pamoja na Alfredina Kaigi, Kiza Mayeye, Nuru Bafadhili, Rukia Kassim, Shamsia Mtamba, Sonia Magogo na Zainab Amir.
Aidha, CUF kimewaapisha wabunge saba badala ya nane kama inavyotakiwa kutokana na mbunge mmoja mteule Hindu Mwenda kufariki siku ya Ijumaa Septemba Mosi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Kwa upande mwingine, wabunge wa upinzani waliingia bungeni baada ya wabunge hao kumaliza kuapishwa na Spika Job Ndugai.
No comments:
Post a Comment