Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya, Wafura Chebukati ametangaza rasmi kuwa uchaguzi wa rais nchini humo utarudiwa kama ilivyoagizwa na mahakama huku akisisitiza kuwa hatajiuzulu nafasi hiyo.
Akizungumza na wanahabari baada ya mahakama ya juu ya nchi hiyo kuufuta uchaguzi uliofanyika Agosti 8, mwaka huu, Chebukati amesema tume hiyo ndicho chombo pekee chenye mamlaka kikatiba ya kuendesha uchaguzi na si vinginevyo.
Amesema tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi mpya ulioamriwa kufanyika ndani ya siku 60, itatangazwa ndani ya siku chache zijazo.
Kuhusu yeye na wenzake katika tume hiyo kuachia ngazi, Chebukati amesema haoni sababu ya kujiuzulu huku akimtaka mkurugenzi wa mashtaka (DPP) kwenda kwenye tume hiyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wake ili kujiridhisha endapo kulikuwa na ukiukwaji wa sheria kama ilivyoelezwa na mahakama.
Amesisitiza kuwa zoezi la upigaji kura halikuwa na kasoro zozote za kisheria na kusema, "Uamuzi wa mahakama umejikita zaidi kwenye zoezi la kutangaza matokeo na siyo zoezi la upigaji kura,”
Licha ya kusisitiza kuwa uchaguzi huo ulifuata sheria, Chebukati amesema atalazimika kuifanyia mabadiliko madogo tume hiyo kutokana na dosari chache zilizobainika wakati wa utoaji wa matokeo.
No comments:
Post a Comment