MWANAMKE mwenye umri wa miaka 25 Ijumaa alishtakiwa kwa kueneza chuki za kikabila akidai “mauaji ya kikabila dhidi ya makabila ya Kikuyu na Kalenjin ndiyo dawa ya kuponya nchi hii.”
Bi Olivian Nyabwazi Moraira Kababa almaarufu Kabz Nyar Kisii alikabiliwa na shtaka la kueneza chuki ya kikabila.
Iwapo mshtakiwa atapatikana na hatia kama alivyoshtakiwa atahukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani.
Shtaka dhidi ya Nyabwazi lasema alisambaza ujumbe wa chuki ya kikabila katika mtandao wake wa Facebook Kabz Nyar Kisii akisema “mauaji ya halaiki ndiyo dawa itakayoponya nchi hii.
Hatuwezi kutawalwa na watu wawili waliolaaniwa, wezi, wauaji na wanyakuzi wa mashamba kutoka kwa makabila mawili kwa zaidi ya miaka 55:”
Kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha alimweleza hakimu mkuu katika mahakama ya Nairobi Bw Francis Andayi kwamba ujumbe huo wa chuki ulilenga kuchochea uhasama dhidi ya makabila ya Kikuyu na Kalenjin.
Bw Naulikha alisema ujumbe huo umenuiwa kuchochea makabila 39 ya Kenya dhidi ya makabila ya Kikuyu na Kalenjin.
Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema ni haki yake.
“Naomba hii mahakama isimwachilie mshtakiwa kwa dhamana kwa sababu adhabu ya kosa analodaiwa alifanya ni kali,” alisema Bw Naulikha.
Hakimu alifahamishwa kifungo hicho ni kishawishi kikubwa cha mshtakiwa kuchana mbuga.
“Mshtakiwa atatoroka akiachiliwa kwa dhamana. Naomba korti imnyime dhamana,” alisema kiongozi wa mashtaka.
Lakini mshtakiwa alipinga matamshi hayo akisema kiongozi wa mashtaka hajawasilisha sababu zozote za kuwezesha mahakama kumnyima dhamana.
Aliomba korti itumie uwezo na kumwachilia kwa dhamana akisema “ni haki ya kimsingi kama invyoamriwa katika Kifungu nambari 49 cha katiba.”
Bw Andayi aliamuru mshtakiwa alipe dhamana ya Sh200,000. Hakimu aliorodhesha kesi hiyo isikizwe Oktoba 3, 2017.

No comments:
Post a Comment