ZIARA YA RAIS KENYATTA KAUNTI YA KILIFI NI FAIDA KWANGU - KINGI

Gavana wa ODM Kaunti ya Kilifi, Amason Kingi, amesema kuwa ziara ya Rais Uhuru Kenyatta na kikosi chake cha Jubilee katika kaunti hiyo kusaka kura itamuongezea umaarufu kuchaguliwa tena kuhifadhi kiti chake mnamo Agosti 8.

GAVANA wa ODM Kaunti ya Kilifi, Amason Kingi, amesema kuwa ziara ya Rais Uhuru Kenyatta na kikosi chake cha Jubilee katika kaunti hiyo kusaka kura itamuongezea umaarufu kuchaguliwa tena kuhifadhi kiti chake mnamo Agosti 8.

Jubilee ikiongozwa na kinara wake Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto Jumatano imeelekeza kampeni za kuvutia ngoma upande wake kwa kipindi cha lalama salama katika Kaunti ya Makueni na Kilifi.

Hata hivyo Gavana wa Kilifi Kingi amekaribisha ziara ya kiongozi huyu wa taifa katika kaunti yake akihoji inaendelea kumpa nafasi murwa ya kuibuka mshindi kuhifadhi kiti chake cha ugavana mnamo Jumanne siku kuu ya uchaguzi mkuu mwaka huu wa 2017, akisema kuwa Rais Kenyatta anapotembea kaunti hiyo huwa hakosi kutaja jina lake.

"Rais atakuwa Kilifi leo (Jumatano) na hiyo ni faida kuu kwangu. Kwenye hotuba yake huwa hakosi kutaja jina langu, na hiyo ni mbinu bora ya kunipigia debe na kunifanyia kampeni," amesema Gavana Kingi Jumatano akifanya kampeni zake Kilifi wakati akihutubia wapiga kura.

Amesema Rais Kenyatta ni 'kampeina' wake mkuu anayemuundia wasifu wa jina lake kwa kumtaja kila anapozuru kaunti yake.

"Leo jina langu litasambaa Kilifi, kwa hivyo nitafanya kampeni maeneo mengine. Jinsi anavyoendelea kuzuru kaunti hii ndivyo kura zangu zinaongezeka," amesema Kingi.

Rais Kenyatta aidha amekuwa akisuta Gavana Kingi pindi anapotembelea Kaunti ya Kilifi akisema kuwa hukosoa serikali ya Jubilee ilhali hajafanya miradi yoyote ya maendeleo katika kaunti yake, na kwamba hutegemea miradi inayozinduliwa na serikali kuu Kilifi.

Akitania Rais, Kingi amesema kuwa Kilifi itapokea idadi kubwa ya watalii kutokana na ziara yake.

Utani

"Utalii huku ulififia serikali ilipotaja Kilifi kuwa ni miongoni mwa kaunti zitakazozuka ghasia wakati wa uchaguzi. Hata hivyo nina imani kuwa ziara ya Rais itaimarisha utalii hapa na hilo ndilo jambo pekee tunalofaidika naye," akasema.

Akaongeza: "Tumekuwa tukiishi kwa amani chini ya utawala wangu, hakuna atakayeuliza yeyote. Mipango ya kusitisha uchaguzi itashindwa kwa njia zote."

Chama cha ODM anachowania kuhifadhi kiti chake nacho, kinaongozwa na kinara wa muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga.

ZIARA YA RAIS KENYATTA KAUNTI YA KILIFI NI FAIDA KWANGU - KINGI ZIARA YA RAIS KENYATTA KAUNTI YA KILIFI NI FAIDA KWANGU - KINGI


Reviewed by KUSAGANEWS on August 02, 2017 Rating: 5

No comments: