Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Arusha imemwachi huru na kufuta shitaka la aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Arusha Lengai Ole Sabaya aliyekuwa anakabiliwa na shitaka la kujifanya mtumishi wa umma katika idara ya usalama wa taifa (TISS).
Mahakama imefuta shitaka hilo baada ya upande wa Jamhuri kuliondoa shitaka hilo mahakamani kwa mara ya nne.
Akitoa taarifa mahakamani hapo wakili wa serikali Pernina Joakimu aliiambia mahakama mbele ya Hakimu Mkazi Nestory Barro akisema upande wa Jamuhuri imeona hakuna haja ya kuendelea na shitaka hilo hivyo anaiomba mahakama ilifute.
Akizungumza baada ya ombi la upande wa Jamhuri Hakimu Mkazi wa Mahakama ya mkoa wa Arusha Nestory Barro ameutaka upande wa Jamuhuri kupitia wakili huyo wa serikali kuacha tabia ya kupeleka shitaka mahakamani na kulitoa kwakuwa ni kinyume na haki za binadamu huku akimtaka wakili wa serikali kusoma vipengele vya sheria vinavyo ahinisha ukomo wa mtu binafsi au taasisi yoyote kumsumbua mtu mara kwa mara kwa kufikisha mahakama na kumwachia bila sababu za msingi.
Akizungumza nje ya Mahakama Lengai Ole sabaya ambaye pia ni diwani wa kata ya Sambasha kwa tiketi ya CCM amesema anaishukuru mahakama kwa kumpa haki kwakuwa yote hayo yanatokana na chuki za kisiasa.
Kwa upande wa wananchi waliomsindikiza Sabaya mahakamani hapo wameishukuru mahakama kwa kumtendea haki kiongozi Wao kwa kuwa walikuwa wanakosa amani.
No comments:
Post a Comment