Watanzania watakiwa kulinda viwanda

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema ujenzi wa viwanda ni jambo linalohitajika, lakini kuvilinda ni muhimu zaidi.

Akizungumza Sabasaba katika ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS), alilitaka shirika hilo kutoruhusu kuingia nchini bidhaa ambazo hazina ubora.

“Viwanda vinaongeza ajira na bidhaa zinapouzwa kwa wingi mapato yanaongezeka. Viwanda vya saruji vipo vingi kwa sasa hatupati tabu ya kuagiza saruji, hivyo kazi kubwa ni kuvilinda kwa kuzuia bidhaa zisizo na ubora.

“Kutokana na kukua kwa kasi ya ujenzi tunapaswa kujiuliza kuhusu changamoto zilizopo kwenye sekta ya ujenzi, je majengo ni sehemu salama kwa wakazi na wajenzi, je kuna hatua zinazohakikisha usalama kwenye sehemu za ujenzi, je malighafi na vifaa vya ujenzi vimethibitishwa kukidhi vigezo na ubora unaotakiwa,” alihoji Mwijage.

Mkurugenzi wa upimaji na huduma ya vifungashio kutoka TBS, Agness Mneney alisema: “Ni muhimu kuzingatia usalama wa wakazi na hata wapita njia katika majengo marefu ambayo hayazingatii vifaa vyenye ubora.

“TBS jukumu letu kubwa ni kuhakikisha vifaa vimepimwa na kupitishwa lakini viwe na ithibati kutoka kwetu, Tanzania TBS ipo moja tu hakuna mamlaka au taasisi nyingine inayopitisha vifaa au bidhaa isipokuwa TBS,” alisema.

Ofisa Ujenzi kutoka TBS, Joseph Kadenge alisema umuhimu wa kupima vifaa vya ujenzi ni kuhakikisha ubora na kuongeza ushindani katika soko.


Watanzania watakiwa kulinda viwanda Watanzania watakiwa kulinda viwanda Reviewed by KUSAGANEWS on July 09, 2017 Rating: 5

No comments: