Madiwani CUF walaani agizo la kumweka ndani Halima Mdee

Diwani wa kiwalani Mussa Kafana (Katikati) akizngumza na wanahabari katika ofisi za wabunge wa CUF zilizopo Magomeni Jijini Dar es salaam

Madiwani 19 wa Chama cha CUF Mkoa wa Dar es Salaam, wamelaani hatua ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi ya kuagiza polisi kumkamata na kumweka ndani kwa saa 48 mbunge wa Kawe, Halima Mdee kwa madai ya kutoa kauli za kashfa kwa Rais na uchochezi kwa Taifa.

Mdee ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) alikamatwa jana (Julai 4) na polisi na kuwekwa ndani kwa amri hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake leo (Julai 5), diwani wa Kiwalani, Mussa Kafana amewaambia waandishi wa habari kuwa kwa niaba ya chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam wamesikitishwa na hatua hiyo.

"Tumeamua kulisema kwa uchache kwa sababu tumepata fursa. Tunalisema kwa sababu linatugusa, Mdee (Halima) ni sehemu ya madiwani na mjumbe wa Baraza la Jiji la Dar es Salaam," amesema.

Kafana ambaye pia ni naibu meya wa Jiji la Dar es Salaam, amesema alichofanyiwa Mdee ni ukiukwaji wa haki za binadamu kwa sababu kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake.

"Sasa hivi imekuwa tofauti ukisema jambo linaloenda kinyume cha mtu fulani unakamatwa unawekwa ndani. Taifa linakoenda siko, ndiyo maana tunalaani na hatukubaliani na kitendo hiki," amesema Kafana.

Madiwani CUF walaani agizo la kumweka ndani Halima Mdee Madiwani CUF walaani agizo la kumweka ndani Halima Mdee Reviewed by KUSAGANEWS on July 05, 2017 Rating: 5

No comments: