Diwani wa Chadema, kata ya Bangata wilayani Arumeru (Arusha)
Emmanuel Mollel amejiuzulu nafasi yake ikiwa ni siku chache baada ya kutuhumiwa
na uongozi wa chama hicho kwa utovu wa nidhamu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Christopher Kazeri
amethibitisha taarifa za kujiuzulu kwa diwani huyo na kusema kwamba ofisi yake
imepokea taarifa za kujiuzulu kwake.
Mollel alipotafutwa kwa njia ya simu leo, Juni Mosi, 2017,
alikiri kuandika barua ya kujiuzulu huku akisema kwamba amefanya uamuzi huo kwa
utashi wake binafsi lakini akakanusha kupewa barua yoyote ya onyo na
uongozi wa chama hicho.
Katibu wa Chadema mkoani Arusha,Aman Gorugwa amethibitisha
taarifa za kujiuzulu kwa kiongozi huyo na kusema kuanzia leo Mollel sio
mwanachama wa Chadema tena.
Gorugwa amesema kwamba uongozi wa chama chao ulimwandikia
barua hivi karibuni ya kumtaka ajieleze sababu za kutowajibishwa kutokana na
tuhuma zinazomkabili.
Ametaja tuhuma hizo kuwa ni pamoja na utovu wa
nidhamu,mwenendo usiofaa ,kwenda kinyume na maagizo ya chama na usaliti.
Amesema hata kabla ya kujibu tuhuma hizo walipokea barua ya
kujiuzulu kwake
Katibu huyo amesema kwamba jina la Mollel lilikuwa kwenye
orodha ya kitabu cheusi (black book) na alikuwa kwenye hatua za mwisho za
kutimuliwa.
Diwani wa Chadema Arusha ajiuzulu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
June 01, 2017
Rating:

No comments:
Post a Comment