UMOJA
wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM), umesikitishwa na vitendo vya
wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) bungeni
muda mfupi kabla ya Rais Dk. Magufuli kulifungua rasmi Bunge la 11
mwishoni mwa wiki.
Wabunge
hao wa Ukawa waliwazomea baadhi ya viongozi walioongozana na Rais Dk.
John Magufuli na kuamriwa na Spika wa Bunge Job Ndugai watoke nje.
Wabunge
hao wa upinznai walifanya hivyo kama hatua ya kutokubaliana na
kufutwa Uchaguzi wa Zanzibar na kutaka atangazwe Maalim Seif Sharif
Hamad kama mshindi wa uchaguzi huo wa Oktoba 25, mwaka huu.
Taarifa
iliyotolewa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka,
ilieleza kuwa kitendo hicho ni cha kuhuzunisha na kufedhehesha.
“Kilichofanyika
ndani ya ukumbi wa Bunge si tabia na desturi njema… Bunge si jukwaa la
vituko au maigizo bali ni eneo lenye kujenga na kuonyesha ukamilifu na
ustawi wa demokrasia na umakini wa kila mbunge na vyama vyao,” alisema
Shaka.
Alisema
UVCCM inaona kitendo hicho kama kielelezo cha ukomo na upeo wa hekima
za wabunge ambao wameaminiwa na wananchi kuwawakilisha kwenye moja ya
mihimili ya dola.
“Tukio
lile ni ishara na dalili tosha ya wabunge wa Kambi ya Upinzani kuwa
hawana dhamira njema ya kuijenga nchi, kupigania maendeleo ya Taifa wala
kuheshimu dhamana na amana waliyokabidhiwa na wananchi kwa njia ya
demokrasia ya uchaguzi,” alisema Shaka.
Alisema ni aibu iliyovuka mipaka kwa wabunge na vyama vyao kufanya kitendo hicho huku.
Alidai kitendo hicho kinaonyesha wabunge hao kupungukiwa ukomavu wa siasa, uwerevu, maarifa na busara za kutosha.
“UVCCM
tunawaomba Watanzania kukitazama kitendo hicho na kukiona kama mwanzo
wa harakati za kuzorotesha maendeleo na kasi ya mafanikio iliyopangwa na
serikali ya awamu ya tano,” alisema Shaka.
Alisema wanaamini viongozi na vyombo husika vitajipanga kukabiliana nao kuzuia aibu kama hiyo isiendelee kutokea.
UVCCM pia umempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa hotuba aliyoitoa katika uzinduzi rasmi wa Bunge la 11, Dodoma.
“Hotuba
ya Rais Dk. Magufuli licha ya kuwa na umakini, matarajio, matumaini,
mwelekeo, dira na vipaumbele muhimu pia imebeba malengo mahususi
katika kuwatumikia wananchi ikiwamo kuimarisha huduma za jamii,
maendeleo ya sekta ya utawala bora, haki na demokrasia, kudumisha
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na uhusiano wa kimataifa,” alisema
Shaka.
UVCCM Wakerwa na Tabia ya Wabunge wa UKAWA Kuwazomea Viongozi wa Kitaifa
Reviewed by KUSAGANEWS
on
November 23, 2015
Rating:
No comments:
Post a Comment