MATANGAZO ya moja kwa moja ya Bunge la 11 yaliyokuwa yakirushwa jana kutoka mjini Dodoma ambapo Spika alitaja jina la Waziri Mkuu wa Serikali wa Awamu ya Tano kuwa ni Kassim Majaliwa (pichani) yalisababisha vifijo na nderemo kwa wananchi wa Kijiji cha Nandagala mkoani Lindi alikozaliwa waziri mkuu huyo anayeapishwa leo.
Baada ya ndugu na majirani kusikia uteuzi wa jina la Waziri Mkuu huyo, kaka wa waziri huyo, Said Hanga, alichukua baiskeli yake na kwenda vijiji vya jirani kuwataarifu uteuzi huo na kisha wananchi walikusanyika na kuanza kucheza ngoma ya Kimwera kushangilia uteuzi huo. Wakizungumzia furaha yao, wanakijiji na ndugu wa waziri huyo walisema hawakutarajia ndugu yao kupewa wadhifa huo mkubwa.
“Nimefurahi sana, sikutegemea mdogo wangu atapata wadhifa huu mkubwa. Niliposikia uteuzi wake kwenye TV, nilichukua baiskeli yangu kwenda kutoa taarifa vijiji jirani na watu walikusanyika kwa furaha na kucheza ngoma,” alisema Hanga.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Msingi Nnacho kijijini hapo, Athumani Mchopa alisema uteuzi wa Waziri Majaliwa ni heshima kwao kwani alimfundisha waziri huyo kuanzia darasa la tatu hadi saba mwaka 1972-79.
“Nimefurahi mwanafunzi wangu kuleta heshima. Nilimfundisha Majaliwa hata masomo ya jioni kwa sababu alikuwa ana maendeleo mazuri darasani. Nilimchukua na kuishi naye nyumbani huku nikimfundisha masomo ya jioni hadi alipofaulu kwenda sekondari,” alisema Mwalimu Mchopa.
Alisema Majaliwa alikuwa na uwezo mzuri darasani na kwamba taarifa za uteuzi wake alizipata kutoka jijini Dar es Salaam kwa ndugu yake aliyemtaarifu uteuzi wa mwanafunzi wake huyo kwa njia ya simu.
Alisema matunda yake yameonekana, kwani Waziri huyo aliibadilisha Namdagala na wilaya yote na kwamba uteuzi huo ni chachu ya maendeleo kwa Taifa na Mkoa wa Lindi.
Mkazi wa Nandagala, Mohammed Vitus alisema Rais John Magufuli ametimiza ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni kijijini hapo kwamba Ruangwa itapata zawadi.
Naye Diwani wa kata hiyo, Andrew Chikongwe (CCM), alisema uteuzi wa Majaliwa umeiletea heshima kata hiyo na kwamba maendeleo ya Ruangwa kiuchumi yanaanza kuonekana na umaskini utapungua.
Alisema miaka mitano ya nyuma, Waziri huyo alipokuwa Naibu Waziri wa Tamisemi ameleta umeme na maji, hivyo uteuzi wake ni kielelezo kwamba rais anaweza kufanya naye kazi kwa vile ni mtendaji.
Aliwashauri wakazi wa Ruangwa kuondoa tofauti zao na kumpa ushirikiano Waziri Mkuu Mteule ili alete maendeleo zaidi ya hapo na kutumia fursa zilizopo.
Mwenyekiti wa Kijiji Garus Nnunduma, alisema amepokea kwa furaha uteuzi huo kwa mkazi wao kupata wadhifa huo mkubwa katika uogozi wa nchi na kwamba hiyo inathibitisha uwezo wake wa kazi. Jukwa
SHANGWE NA VIGELEGELE ALIPOZALIWA WAZIRI MKUU MAJALIWA
Reviewed by KUSAGANEWS
on
November 20, 2015
Rating:
No comments:
Post a Comment