MAJALIWA AWATAKA WABUNGE WASITAFUTE MCHAWI

WAZIRI Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, amesema uchaguzi umekwisha na kuwataka wabunge waende wakashirikiane na wananchi kufanya kazi badala ya kutafuta mchawi.
Akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 11 bungeni mjini Dodoma jana, Waziri Mkuu, alisema wabunge wanalo jukumu kubwa la kuishauri serikali ili kuhakikisha matatizo na kero mbalimbali za wananchi zinatatuliwa.
Aliwaeleza wabunge kuwa wamepata kura nyingi zilizowawezesha kupata ushindi mwaka huu na kwamba kazi ya kutafuta kura za mwaka 2020 wanaianza sasa kwa kufanya kazi ya uwakilishi wa wananchi kwa umahiri mkubwa. “Mwito wangu kwenu Waheshimiwa wabunge ni kwamba sasa wote kwa pamoja tushirikiane na serikali na wananchi waliotuchagua kujenga nchi yetu. Masuala ya makundi ya kisiasa kati yetu sasa yaishe na tufanye kazi kwa maendeleo ya Taifa,” alisema Waziri Mkuu.
Pia alisema ni matarajio ya serikali kuwa itapata taarifa na ushauri kutoka kwa wabunge juu ya maeneo yanayohitaji kupewa msukumo ili kuongeza kasi ya maendeleo ya Taifa.
“Kwa upande wa Serikali itafanyia kazi taarifa na ushauri huo lengo ikiwa ni kuitoa Tanzania kutoka kwenye dimbwi la uchumi ulio nyuma na tegemezi na kuiingiza katika mkondo wa uchumi imara, endelevu unaokua na wa Taifa linalojitegemea. Jukumu hilo ni letu sote,” alisema Majaliwa.
Aliwataka wabunge waende majimboni mwao waanze kazi kwa bidii, ushirikiano na upendo na kwamba kila mmoja akifanya kazi kwa kujituma, ana imani Taifa litasonga mbele na maisha yatabadilika.
“Tukitaka kusonga mbele kwa mafanikio lazima tuweke dhamira ya kweli na tukomae nayo kwa kufanya kazi zaidi na kwa bidii zote. Mheshimiwa Rais ameshatupatia nguvu mpya ya kwamba ‘Hapa Kazi tu’ tuweke dhamira pasiwe na yeyote wa kuturudisha nyuma.
“Narudia kuwaombeni kwamba sasa uchaguzi umekwisha, wote tuseme kwa dhamira moja, yaliyopita si ndwele tugange yajayo, twendeni sasa tukashirikiane na wananchi kufanya kazi. “Turejeshe ushirikiano na mshikamano, tuwasaidie na kuwaongoza wananchi kutatua matatizo yao, tusibaki tunatafuta mchawi,” alisema.
Pia aliwaomba watumishi wote wa serikali kutoa ushirikiano katika kutekeleza ahadi za Rais Magufuli, wakati na baada ya kampeni, ilani ya Chama Cha Mapinduzi na Dira ya Maendeleo ya Taifa na wafanye kazi kwa bidii kuwatumikia Watanzania kwa kasi na umakini wa hali ya juu.
Mkutano huo wa kwanza wa Bunge la 11 ulianza Jumanne wiki hii, ambapo pamoja na mambo mengine ulichagua Spika, Naibu Spika, kuapisha wabunge na kuthibitisha jina la Waziri Mkuu. Bunge limeahirishwa hadi Januari 26 mwakani.



MAJALIWA AWATAKA WABUNGE WASITAFUTE MCHAWI MAJALIWA AWATAKA WABUNGE WASITAFUTE MCHAWI Reviewed by KUSAGANEWS on November 20, 2015 Rating: 5

No comments: