Chadema na Polisi Wavutana Msiba wa Mawazo.....Polisi Wapiga Marufuku Watu Kukusanyika Kuuaga Mwili wa Marehemu Wakihofia Kipindupindu
Serikali wilayani Geita na Polisi Mkoa wa Mwanza, wamepiga marufuku wanachama na wafuasi wa Chadema kukusanyika kwa ajili ya kuaga mwili wa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo (pichani).
Akizungumza ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo alisema wamezuia mikusanyiko ya aina yoyote kutokana na kuwapo kwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.
Shughuli hizo za kuaga mwili zimepangwa kufanyika kati ya leo na kesho kwenye Viwanja vya Furahisha, au ofisi za Chadema Kanda ya Ziwa.
“... hatukubali mikusanyiko yoyote kutokana na kuwapo mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu. Kama ulinzi wa kusindikiza mwili kutoka Bugando hadi Geita tutawapatia ili wakafanyie taratibu za mazishi huko siyo hapa, ” alisema.
Mkumbo alisema kutokana na mikusanyiko hiyo, yapo makundi yamejipanga kutumia mwanya huo kufanya uhalifu.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Nyamagana, Japhet Nungwana alisema tayari walikuwa wameomba Uwanja wa Nyamagana kufanya ibada ya kumuaga Mawazo.
Alisema hawajapokea taarifa yoyote ya kuzuia mikusanyiko hiyo na kwamba, kama wataona siyo vizuri kutumia uwanja wao watafanyia ibada katika ofisi zao za Kanda.
“Hatuendi kufanya vurugu au mkutano, tunafanya ibada ya kumuaga ndugu yetu ila wakituzuia uwanja wao tutatumia ofisi zetu za Kanda,”alisema Nungwa na kuongeza:
“Hatuwezi kuacha kumuaga kwani yule alishawahi kuwa kiongozi mkoani hapa, hivyo kushindwa kufanya ibada ya kumuaga tutakuwa hatujatenda haki. Iwapo wanazuia kwa sababu ya kipindupindu kwa nini hawajazuia ibada na mikusanyiko ya watu misikitini au makanisani?”
Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza, Onesmo Rwakyendela alisema kwa takriban miezi miwili, wamepata wagonjwa 422 wa kipindupindu na 18 wamepoteza maisha.
“Kwa sasa Wilaya ya Ilemela ina wagonjwa watano, Sengerema na Ukerewe mmoja mmoja, niwatake wananchi kutofanya mikusanyiko isiyo ya lazima maana huwezi kujua nani ana vimelea vya ugonjwa huo,” alisema Dk Rwakyendela.
Geita pia Marufuku
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie amepiga marufuku shughuli ya kuaga mwili huo iliyokuwa imepangwa kufanyika kesho akisema Mawazo si kiongozi wa kitaifa wala mkazi wa mjini hapa.
Akizungumza ofisini kwake jana, Mangochie alisema: “Hapa hana nyumba wala siyo kiongozi wa kitaifa, hivyo msiba wake unatakiwa upelekwe nyumbani siyo kuagwa kwenye eneo la hadhara, hapa siyo kwake.”
Alisema ameona kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook mtu mmoja akitoa taarifa za mazishi kuanzia Mwanza halafu Geita na kwamba, hiyo siyo sahihi na amepiga marufuku shamrashamra zote kwenye msiba huo.
Hata hivyo, Katibu Msaidizi wa Chadema wa Jimbo la Geita, George Anthony alisema chama hicho hakijapata taarifa za zuio hilo na kwamba wametimiza taratibu zote za kuomba kibali polisi na Serikali walipewa.
“Tumekabidhi barua na kuongea nao ana kwa ana wameturuhusu na kutupa Uwanja wa Magereza, sasa sisi ratiba yetu ya kumuaga Jumapili ipo palepale huyu ni kiongozi wa mkoa na kitaifa wananchi wana haki ya kumuaga,” alisema Anthony.
Alisema ratiba yao inaonyesha kuwa ataagwa mjini Geita na baadaye Katoro, kisha kijijini kwake Chikombe.
DC alaani mauaji
Awali, Mangochie alisema Serikali ilipokea kwa masikitiko msiba huo na kulaani mauaji hayo ya kinyama na kikatili.
“Nitoe pole kwa familia ya Mawazo pia kwa chama, kwa kuondokewa na kiongozi wake mimi na viongozi wenzangu tumepokea kwa masikitiko makubwa, nalaani kitendo kisichokubalika cha kumshambulia na kusababishia kifo,” alisema.
Alisema zipo taarifa za upotoshaji wa kifo hicho zinazotolewa ambazo siyo za kweli, hivyo kuwataka wananchi kuachana nazo na kusubiri taarifa za uhakika kutoka polisi.
Mpekuzi
Chadema na Polisi Wavutana Msiba wa Mawazo.....Polisi Wapiga Marufuku Watu Kukusanyika Kuuaga Mwili wa Marehemu Wakihofia Kipindupindu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
November 21, 2015
Rating:
No comments:
Post a Comment