wandishi wa habari watakiwa kufuata maadili ya kazi zao



 WAANDISHI wa habari nchini, wametakiwa kutekeleza wajibu wao kwa kufuata maadili na misingi ya uandishi wa habari hususan za uchunguzi wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Wametakiwa kuwajibika ipasavyo katika majukumu yao kwa kuwatendea haki wagombea wote pamoja na vyama vyote vya siasa, bila kuegemea upande wowote, ikiwa ni pamoja na kuandika habari za ukweli na kwa usahihi.

Mwito huo ulitolewa jana na mwezeshaji, Chrysostom Rweyemamu, kwenye warsha ya kuhusu Uchaguzi Mkuu Tanzania, inayoshirikisha waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, inayofanyika jijini Mwanza.

Rweyemamu alisema ni wajibu wa waandishi wa habari kufuata misingi ya uandishi wa habari, hasa kuhusu habari za uchunguzi katika kipindi hiki kinachokaribia uchaguzi mkuu. Alisema waandishi wa habari ni vema kabisa wawe makini katika kuandika habari za uchunguzi, ikiwa ni pamoja na kuibua habari zilizojificha ili wananchi wapate ukweli na kuchukua uamuzi sahihi wa kuchagua viongozi bora na wanaofaa na siyo bora viongozi.

“Waandishi wa habari ni vema kabisa muwe makini katika kuandika habari za uchunguzi hasa katika Uchaguzi Mkuu ujao,” alisema. Aliwataka waandishi wa habari wachunguze na kuandika habari zinazohusu udanganyifu wa mali za wagombea zilizotamkwa, kuhusu afya zao, elimu yao, kashfa za rushwa, kumbukumbu za wagombea, kashfa katika ofisi za umma, kumbukumbu za polisi, taarifa za awali, uraia wa mgombea na taarifa za awali.

Aidha, alisema kuwa waandishi wa habari wanatakiwa kuwahi kufika mapema katika eneo la tukio na kuangalia mazingira yalivyo, ikiwa ni pamoja na kuchukuwa tahadhari wakati wakitekeleza majukumu yao ili kulinda maisha yao.

Hata hivyo, alisema kuwa katika kuandika habari za uchunguzi kuna changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kusalitiwa na vibaraka waliolipwa, vyanzo vilivyopandikizwa na vinavyotengenezwa, matatizo ya kisheria, kuingiliamambo binafsi, rushwa, kashfa na kushambuliwa kwa kipigo.

Alisema namna ya kukabiliana na changamoto hizo ni kuwa makini na kufuata maadili ya uandishi wa habari na misingi yote ya uandishi wa habari.
wandishi wa habari watakiwa kufuata maadili ya kazi zao wandishi wa habari watakiwa kufuata maadili ya kazi zao Reviewed by KUSAGANEWS on August 16, 2015 Rating: 5

No comments: