Joseph Butiku: CCM inanuka

 MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amesema wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanahama kutokana na chama hicho kunuka kwa kuendesha mambo kimizengwe.
Amesema kwa muda mrefu chama hicho kimeharibiwa na hata kufikia mazingira yaliyopo sasa, huku akisisitiza kuwa wanachama wake kuhama ni halali kwa kuchoshwa na mizengwe na rushwa, na kwa hivyo wapokewe na vyama vingine.
“Watu wameendelea kuharibu Chama Cha Mapinduzi-chama kimekuwa na mazingira ya kunuka.., tuliiambia CCM mlifanya makosa na ni bora kuwaambia wananchi mmekosea.

“… kule wanakokwenda wasiende wakavuruga kama walikotoka. Juzi nilisema, mkileta uchafu, watu wasiwapigie kura,” amesema Butiku kwenye kongamano la taasisi hiyo lililofanyika mchana Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Kongamano hilo lililenga kujadili umuhimu wa maadili katika kuimarisha amani, umoja na haki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
“Tazameni maslahi yenu, kama hukubaliani na msimamo wa chama, unatoka mara moja, sio kubaki ndani na kuchafua watu halafu unatoka,” amesema akipigilia msumari kwamba kinachoitwa “wanamtandao” ndio kimeharibu chama.

Akizungumzia wanasiasa matajiri, amesema si jambo baya, isipokuwa wasitumie utajiri wao kukandamiza wananchi wengine.

Kwenye kongamano hilo Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Mwesiga Baregu amesema Jeshi la Polisi limefanya kazi nzuri ya kulinda msafara wa mgombea urais wa UKAWA, Edward Lowassa, siku aliyokwenda kuchukua fomu ya uteuzi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Prof. Baregu amesema awali alishituka alipofika Buguruni zilipo ofisi kuu za Chama cha Wananachi (CUF) kwa kukuta umma mkubwa wa wafuasi wa vyama hivyo pamoja na National League for Democracy (NLD) na NCCR-Mageuzi, lakini Polisi wakauongoza msafara na kufika mwisho salama usalimini.

“Nilishituka kwa sababu nilikuta watu wengi wanamsubiri mgombea huku tayari nimesikia tangazo la Polisi kuzuia maandamano, nilijiuliza itakuwaje.

Hata hivyo, kutokana na maoni ya wachangiaji ambao walilaumu mbinu za Polisi kukorofisha vyama vya upinzani, Prof. Baregu aliondoa pongezi zake kwa Polisi aliosikia waziwazi wakilaumiwa kwa upendeleo kwa CCM.

Kuhusu mabadiliko ya siasa za vyama vingi nchini, Prof. Baregu amesema mazingira ya uchaguzi kwa sasa ni tofauti kwani kabla ya mwaka 1995 waliounga mkono vyama vya upinzani ni asilimia 20, leo wimbi la mabadiliko linaonekana dhahiri kutokana na mwamko mkubwa kwa wananchi.

“Asilimia 60-70 ya wapigakura ni vijana ambao wengi wamejiandikisha,” anasema na kuhimiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi isimamie taratibu kwa uwazi na kwa mujibu wa sheria huku ikirekebisha malalamiko badala ya hali iliyoshuhudiwa kwa Mwenyekiti Jaji Damian Lubuva alivyokuwa mkali na akilaumu wanasiasa kuishinikiza tume.

Prof. Baregu anasema, “jana nimekwenda kwenye kituo changu nilichojiandikisha ili nihakiki jina langu, lakini nikaoneshwa maboksi 30 yaliyokuwa na fomu zilizotumika kutuandikisha. Ina maana fomu zile zingalipo kwenye ofisi za Kata hazijaondolewa, “sasa hayo majina yataingizwa lini kwenye daftari la wapigakura.”

Akizungumzia uadilifu ndani ya vyama kwa kusema ni tatizo linalohitaji kurekebishwa.
“Sizungumzii uadilifu katika wagombea, sipo hapa kuhukumu,” amesema. “Rushwa katika uchaguzi imeanza kunyemelea vyama vingine vya siasa.”

Amesema tatizo la kihistoria kutokana na CCM, alichokiita “chama kaka” kuzalisha watu waliohamia vyama vingine baada ya mageuzi.

“Vinaangalia mwenendo wa sasa, na sisi tupo tumeanza kuangukia huko, nazungumza na Watanzania ugonjwa huo ni mbaya na ni wa kuogopa kama ukoma. Imefikia watu wanamwambia mgombea unatuachaje,” amesema.

Prof. Baregu amesema lipo suala la msingi halijazungumzwa vizuri kitaifa, na halijakemewa vilivyo – maadili ya uongozi.
“Hakuna kiongozi serikalini amelizungumzia suala hili zaidi. Mwalimu Nyerere aliliona hili mapema na ndio maana alilikemea kabla ya kufa.

“Na hapa ndipo aliposema Watanzania wanataka mabadiliko, wakiyakosa ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM. Nadhani hapo kwa sasa ndipo tulipo,” amesema.

Akichangia mada ya “Maadili na Uadilifu,” aliyekuwa kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole amesema kama CCM ni chama kaka, basi kwa kuwa anakikosoa, anaamini ni sahihi kuvikosoa vyama vingine.

“Mimi sijali mtu kwa mtu kunipenda kwa sababu nimesimamia naye ama la… hata baba ama mama yangu kama wamekosea nitawaeleza kwa lugha ya mama kwamba ‘mmekosea’” amesema.

Polepole ambaye amejenga msimamo wa kutoona mgombea mzuri kati ya CCM (Dk. John Magufuli) na UKAWA (Edward Lowassa), amesema CCM wakiwapa dhamana watu anaowajua si waaminifu, atazunguka nchi nzima kusema asichaguliwe. “Haikuwa kauli rahisi. Watu wakasema najitafutia matatizo, ni sawa tu simhofii mtu kwa kubaki na ninaloliamini,” amesema.

“Wiki tatu zilizopita, katika ukweli uleule niliokiambia Chama Cha Mapinduzi sasa, kwa kiwango kile kile nimewaambia wadogo wa chama kaka (Chadema-UKAWA) kuwa mimi mmenipenda kwa muda mrefu lakini katika hili mmekosea.”

Kimsimamo, anamuona Lowassa ni sehemu ya uovu uliofanywa na CCM wa kupinga maoni ya wananchi katika utungaji wa Katiba Mpya ya wananchi. Polepole anasema bado ni mwanachama wa kawaida wa chama hicho.
Joseph Butiku: CCM inanuka Joseph Butiku: CCM inanuka Reviewed by KUSAGANEWS on August 16, 2015 Rating: 5

No comments: