Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi
ametangaza kujivua uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema).
Sumbawanga. Mbunge wa Mpanda Mjini,
Said Arfi ametangaza kujivua uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema).
Akizungumza mjini Mpanda
katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi
Kashaulili, mwishoni mwa wiki Arfi aliwaeleza wananchi wa Mpanda kuwa uanachama
wake ndani ya Chadema utakoma mara tu baada ya kuvunjwa Bunge Julai 9.
Pia, alitumia mkutano huu
kuwaaga wananchi wa jimbo hilo akisema hatagombea tena nafasi hiyo
aliyoitumikia kwa miaka 10.
Arfi alifafanua kuwa
hayuko tayari kugombea jimbo hilo kupitia chama chochote cha siasa na kauli
hiyo imelenga kuondoa uvumi uliokuwa umeenea kwamba alikuwa na nia ya kugombea
kupia ama ACT – Wazalendo au CCM.
Alisema amekuwa
akishangazwa na kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya wanachana na
wapenzi wa Chadema kuwa hajafanya lolote kwenye chama hicho.
Alisema kama kuna mtu
anayekifahamu vizuri chama hicho ni yeye, hivyo haoni sababu za watu kumbeza.
Alisema alikuwa ameamua
kukaa kimya na kuwa akiamua ‘atamwaga mboga’ ili watu wafahamu upungufu ulioko
ndani ya chama hicho.
Alisema hagombei katika
jimbo hilo na kama kweli chama hicho kina nguvu, basi kilitetee, akisisitiza
kuwa ana uhakika jimbo hilo litakwenda CCM kwa kuwa wananchi wa Mpanda Mjini
walikuwa na mapenzi na mtu siyo chama.
Arfi aliyewahi kuwa
Makamu Mwenyekiti wa Chadema kabla kujiuzulu wadhifa huo, aliwahi kuhusishwa
kusuka mpango wa kumwezesha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kupita bila kupingwa
katika kinyang’anyiro uchaguzi wa mwaka 2010 katika Jimbo la Katavi kwa
kuwashawishi baadhi ya wagombea kuondoka majina yao.
Hata hivyo, Arfi amekuwa
akikanusha tuhuma hizo, hali ambayo pia ilisababisha kutokuelewana na baadhi ya
viongozi wenzake na kusababisha kujiuzulu nafasi yake ya umakamu mwenyekiti.
Baadhi ya wananchi
waliozungumza na gazeti hili walionyesha kushtushwa na kauli ya mbunge huyo
kujiondoa Chadema lakini wakasema ametimiza haki yake ya kikatiba kuchagua
sehemu iliyo sahihi kwake.
Mmoja wa wananchi hao,
Abdallah Hussein alisema: “Arfi amekuwa mvumilivu sana ndani ya Chadema lakini
anayo ya moyoni sasa kwa muda mrefu amekaa kimya aliogopa ya Zitto Kabwe
yasimtokee, sasa ameweka bayana msimamo wake acha tuheshimu mawazo yake.”
Mbunge ajivua uanachama Chadema..
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 07, 2015
Rating:
No comments:
Post a Comment