MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), umesema
matukio ya kupigwa na kuteswa kwa raia wakiwa mikononi mwa polisi yanaongezeka
siku hadi siku na kuongeza hofu kwa jamii juu ya uwapo wa utawala wa sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es
Salaam, Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, alisema matukio hayo yanaongezeka
huku baadhi ya watu wakitishwa na kuambiwa siyo raia na wengine kunyang'anywa
pasi za kusafiria
Alisema wanalaani vikali vitendo vya karibuni vya ukiukwaji
wa sheria na haki za waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu
kunakofanywa na Jeshi la Polisi lenye wajibu wa ulinzi wa raia na mali zao.
"Tunashuhudia waandishi wakipigwa na kukamatwa na
polisi wakati wakitekeleza majukumu yao ya kazi kwa mujibu wa sheria za
nchi," alisema.
Alisema kuwa Agosti 8, mwaka huu, mwandishi wa habari wa
Wapo Radio, Silas Mbise, alishambuliwa na kukamatwa na polisi akiwa kazini na
alipigwa waziwazi na polisi wenye silaha huku akiwa amelala chini na hana
silaha yoyote
Alisema kuwa tukio lingine la hivi karibuni ni la mwandishi
wa gazeti la Tanzania Daima, Sitta Tuma, aliyepigwa na kukamatwa na maofisa wa
polisi wakati akichukua habari katika mkutao wa kampeni za uchaguzi wa diwani
wilayani Tarime mkoani Mara
THRDC ilitoa msaada wa kisheria ili kumwezesha kupata
dhamana na wakili wake Ernest Muhagama alisema alipofika polisi alielezwa kwa
mtuhumiwa huyo kakamatwa kwa kosa la kuandamana kinyume cha sheria. Aliachiwa
kwa dhamana Agosti 9," alisema
Aliyataja matukio mengine ni ya miezi miwili iliyopita dhidi
ya wa waandishi wa habari kuwa ni yaliyofanywa dhidi ya George Ramadhani na
Christopher Gamaina, waliokamatwa na polisi mkoani Mwanza wakati wakiwa
wanatekeleza majukumu yao na walifunguliwa mashtaka mahakamani
Alisema mwandishi mwingine ni Emmanuel Kibiki aliyekamatwa
na polisi mkoani Iringa na kulazimishwa kulala polisi kwa siku kadhaa kabla ya
kufikishwa mahakamani
"Kwa ujumla, hali ya uhuru wa wanahabari na vyombo vya
kawaida na vya mitandaoni umezidi kutoweka na kupelekea kuzuia Watanzania
kupata habari sahihi na kwa wakati kwa mujibu wa Katiba," alisema
'Kwa sasa, wanahabari wamejawa na hofu kubwa kutoa taarifa
zozote watakazohisi hazitawafurahisha baadhi ya watawala," alisema
"Tunasikitishwa na kuongezeka kwa matukio ya kupigwa na
kukamatwa kwa wanahabari bila sababu za msingi na za kisheria. Wanafanya kazi
katika mazingira magumu kutokana na vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na
polisi," alisema
Kwa mujibu wa Olengurumwa, polisi ni chombo muhimu kinachotakiwa
kusimamia uhuru na usalama wa waandishi wa habari na siyo kuwashambulia kama
ilivyotokea mara kadhaa kwa baadhi ya maofisa wa polisi kutumia nguvu kubwa
kuwashambulia na kuwajeruhi wanahabari wakiwa kazini
"Ni lazima ikumbukwe kuwa kila mtu anayo haki ya ulinzi
kwa mujibu wa sheria za nchi, vyombo vya dola vina wajibu wa kuwalinda raia na
mali zao ikiwemo waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu
Tanzania," alisema
Katika hatua nyingine, THRDC imewapongeza polisi Wilaya ya
Loliondo kwa kuwakamata maofisa wa Kampuni ya Uwindaji ya OBC waliowapiga na
kuwadhalilisha raia katika maeneo yao
"Kwa sasa, wahusika wanashikiliwa na polisi Mkoa wa
Arusha kwa uchunguzi zaidi, kutokana na historia ya Loliondo na mgogoro wake na
OBC swala hili halina budi kupongezwa kwani siku zote polisi walishindwa
kuwalinda watetezi wa haki za binadamu na raia wanapojikuta wana mgogoro na
OBC," alisema
Aliongeza kuwa matukio ya watu kuhojiwa uraia wao yanazidi
kuongezeka na sasa wamefika viongozi na raia saba wanaodaiwa siyo raia licha ya
kuzaliwa na kuishi Tanzania kwa maisha yao yote
Aliwataja viongozi hao kuwa ni pamoja na Askofu wa Jimbo la
Ngara, Severine Niwemugizi, Olengurumwa, Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi
Tanzania, Abdul Nondo, Mkurugenzi wa Twaweza na Aidan Eyakuze
Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Wanawake
Wafugaji (PWC), Maanda Ngoitiko na Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible
Fellowship, Zacharia Kakobe
Matukio kama haya yakiendelea kutokea hasa dhidi ya watetezi
wa haki za binadamu, yataendelea kusababisha hofu na kupoteza uhuru wa watetezi
wa kufanya kazi zao kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi," alisema na
kuongeza
"Matumizi ya nguvu kupita kiasi na kutojali utawala wa
sheria pia vimezidi kuchangia kuzorota kwa hali ya watetezi wa haki za binadamu
nchini
"Baadhi ya vyombo vya dola vinatumia nguvu kubwa
kuingilia uhuru wa asasi za kiraia na watetezi wanapotaka kufanya mikutano ya
ndani na kudai kuwa lazima wawe na vibali au hali ya usalama hairuhusu mikutano
hadi ya ndani
THRCD wakemea Ukatili wa Polisi Kwa Wanahabari
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 13, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment