Rais Dkt. John Magufuli amefanya
mabadiliko madogo ya wakuu wa wilaya pamoja na kuteua wakurugenzi wapya 41 wa
halmashauri za wilaya, miji na manispaa huku akiwahamisha vituo wakurugenzi 19,
kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kujaza nafasi zilizowazi.
Katika mabadiliko hayo, Rais
Magufuli pia amembadilisha kituo cha kazi mkuu wa wilaya ya Kwimba, Mhandisi
Msafiri Simeoni na kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato na kumteua Senyi Simon kuenda
kushika nafasi yake.
Akisoma uteuzi huo Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi John Kijazi amewataka wakurugenzi wote wapya kuripoti siku ya
Jumatano, Agosti 15, 2018 katika ofisi za Katibu Mkuu wa TAMISEMI pia
watakapokwenda Dodoma wanapaswa kuwa na vyeti vyao vya kidato cha nne, sita na
elimu ya taaluma.
"Wakurugenzi ambao katika
mabadiliko haya wamebadilishwa vituo vya kazi, wanapaswa kwenda kuripoti katika
vituo vyao vya kazi mara moja. Na kwa wale wakurugenzi walioteuliwa kwa mara ya
kwanza wanatakiwa kuripoti kwa Katibu Mkuu wa TAMISEMI Agosti 15 mwaka huu kwa
ajili ya kiapo cha uadilifu na maelekezo ya majukumu yao", amesema Balozi Kijazi.
Mbali na hilo, Rais Magufuli
amemuamisha kituo cha kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa Kakonko Mkoa wa Kigoma
Lusubilo Mwakabili na kuwa mkurugenzi wa halmashauri ya Temeke. Pia amemteua
Beatrice Kwai kuwa mkurugenzi wa halmashauri ya Ubungo na Mwilabu Nyabusu
amemteua kuwa mkurugenzi wa halmashauri ya Kigamboni.
Uteuzi huo wa Rais Magufuli unakuwa
wa pili kufanyika kwa kufanya mabadiliko makubwa katika safu ya uongozi ambapo
wa kwanza ulikuwa ni Julai 28, 2018 ambapo aliteua wakuu wa mikoa, wilaya
pamoja na makatibu tawala.
Rais Magufuli apangua safu za wakurugenzi
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 13, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment