Mbunge CUF Ataja sababu za kujiunga na CCM

Mbunge wa Liwale (CUF) Zuberi Kuchauka ametaja sababu tatu za kurejea CCM

Akizungumza leo Jumatatu Agosti 13, 2018 katika ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini hapa baada ya kutambulishwa na Katibu Mkuu wa chama hicho tawala, Dk Bashiru Ally, Kuchauka amesema moja ya sababu ni mgogoro ndani ya CUF

Amesema sababu nyingine ni CCM kuwa na mabadiliko katika kipindi cha miaka 10 iliyopita pamoja na utekelezaji wa ahadi mbalimbali za uchaguzi

Kuchauka ametangaza kurejea CCM ikiwa zimepita siku mbili tangu Julius Mtatiro, aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la uongozi CUF upande unaomuunga mkono katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, naye kuhamia CCM.

Katika ufafanuzi wake Kuchauka amesema ndani ya CUF alijikuta katika wakati mgumu kutokana na mpasuko hatua iliyoathiri utekelezaji wa majukumu yake ya kibunge.

“Sasa hivi mtu akisema CUF unaulizwa ni CUF gani? Mtaona namna gani tulivyopoteza mwelekeo, mimi nimechaguliwa na wananchi. Ukisimama kwenye jukwaa la CUF ya Lipumba (Profesa Ibrahim-mwenyekiti wa CUF  anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa)   unaonekana msaliti,” amesema.

“Na ukionekana jukwaa la CUF Maalim unafukuzwa kwenye chama. Kwa hiyo unakosa utulivu na nikaona  sina sababu ya kuendelea kubakia kwenye hali ya wasiwasi.”

Katika sababu yake nyingine Kuchauka amesema CCM ya sasa si ya mwaka 2005, ina mabadiliko mengi.

“Ile ya 2005 ilikuwa inapoteza mwelekeo lakini CCM hii chini ya Rais Magufuli (John) nimeikubali kwa kuwa inarejea kwenye misingi ya TANU. Mimi kama mpenda maendeleo sikujutia kurejea,”amesema.

Amesema kutokana na mazingira hayo hakuona haja ya kuchelewa kuchukua uamuzi wa kujiunga na chama hicho tawala.

“Kwa hivyo mimi kama mbunge wa Liwale nikakuomba (Dk Bashiru) nije kwenye ofisi yako nitamke kwamba kuanzia sasa hivi mimi si mwanachama tena wa CUF. Nyadhifa nilizozipata nikiwa CUF zitakuwa zimeondoka,” amesema.<

Amesema sababu nyingine ni utekelezaji wa ahadi za uchaguzi zilizotolewa na chama hicho tawala.

"Tumepata Sh1bilioni kwa ajili ya kujenga hospitali, tumepata watumishi 80 wa afya. Kuna migogoro mingi, nimetembelewa na mawaziri sita, watu walidhani wakichagua upinzani hatutatembelewa na mawaziri," amesema

Mbunge CUF Ataja sababu za kujiunga na CCM Mbunge CUF Ataja sababu za  kujiunga na CCM Reviewed by KUSAGANEWS on August 13, 2018 Rating: 5

No comments: