Mavunde ataka wawekezaji kutotumia mawakala kuomba vibali


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde amewataka wawekezaji nchini kuacha kutumia mawakala wanapotaka vibali mbalimbali

Waziri Mavunde ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Agosti 13, 2018 wakati akizungumza kwenye mkutano ulioandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na wafanyabiashara wenye asili ya China
Wawekezaji hao walikuwa na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika utendaji wa shughuli zao hapa nchini

“Hakuna kibali cha kufanya kazi au kuishi kinachotolewa zaidi ya siku 14, mnatumia mawakala kuwaombea vibali ndiyo maana anapata majibu tofauti,” amesema Mavunde

"Nendeni wenyewe kwenye ofisi husika na iwapo mmejaza fomu vizuri na mkaambatanisha kila kinachohitajika na ikachukua zaidi ya wiki mbili njooni kwangu.”

Kuhusu muda wa wageni kufanya kazi kabla ya kuwaelekeza wazawa shughuli husika na kuondoka, Mavunde amefafanua kuwa ni suala la kisheria ambapo ikimalizika miaka mitano anapaswa kuondoka
"Ipo nafasi ya kukatiwa rufaa baada ya muda huo kama hiyo nafasi ni muhimu na hakuna Mtanzania anayeweza kuifanya,” amesema

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Group Six International,  Marco Lee amesema kuwa suala la kuwasilisha vyeti vya taaluma wakati wa kuomba vibali vya kufanya kazi nchini haoni kama lina maana

Amesema anachofahamu wapo watu wana ujuzi na hawajasomea kazi husika, hivyo ni bora waangalie ujuzi na uzoefu badala ya vyeti
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dk Aggrey Mlimuka amesema kuwa watahakikisha waajiri wa ndani na nje ya nchi wanazijua sheria za ajira na ndio maana wameandaa mkutano huo.
Mavunde ataka wawekezaji kutotumia mawakala kuomba vibali Mavunde ataka wawekezaji kutotumia mawakala kuomba vibali Reviewed by KUSAGANEWS on August 13, 2018 Rating: 5

No comments: