Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema chama hicho
kimejipanga kuondokana na siasa za kusifu mtu.
Alisema hayo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano na
waandishi wa habari kuzungumzia mafanikio ya chama chake katika uchaguzi mdogo
wa udiwani katika kata 77 na ubunge wa Jimbo la Buyungu
Baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzani wakiwamo wabunge
na madiwani ambao wanavihama vyama vyao na kujiunga na CCM wengi wamekuwa
wakieleza sababu kuwa ni kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli
Akijibu maswali ya waandishi wa habari jana kuhusu suala
hilo, Dk Bashiru alisema CCM ni chombo chao na Tanzania ni yao.
“Kama ambavyo
Tanzania itakuwapo bila Magufuli na CCM itakuwapo bila Magufuli. Kama ambavyo
ipo bila Mzee Karume na Mzee Nyerere. Tupo na mimi hapa nipo. CCM chini ya
Bashiru, chini ya Kinana, chini ya Makamba, chini ya Mangula, chini ya Mkama
ipo,” alisema Dk Bashiru
Alisema, “Tunataka kuua siasa za ubinafsi, za nafsi moja, za
mtu mmoja na Rais Magufuli hapendi kutajwa kama mtu mmoja, hapendi majivuno na
hawezi kuwa na majivuno ndani ya CCM. Akiwa na majivuno amepoteza sifa na sifa
kubwa inayompamba na kukipamba chama chetu ni mtu wa watu anayeleta maendeleo
kwa watu na yeye ni mtu. Kwa kuwa ni mtu, atakuwapo na hatakuwapo.”
Dk Bashiru alipoulizwa ni kwa nini wasiwaambie wahamiaji wa
CCM kufuta kauli hiyo alisema haiwezekani kwa kuwa Rais Magufuli ndiye mshika
chombo
“Chombo kitakwenda mrama. Anasifiwa mwendesha chombo kwa
sababu chombo chenyewe ni madhubuti na amehimili usukani. Ukifunga bao,
unasifiwa wewe, timu inapata sifa,” alisema
“Tunataka kuua utaratibu wa siasa za kusifu mtu, mwenyekiti
wa chama kile au hiki, akiondoka kinadondoka naye. Tunataka kiongozi na sifa za
kiongozi lazima zielekeze kwake kwa niaba ya anaowaongoza. Ukiona sifa zake kwa
anaowaongoza pia wanakuwa nazo,” alisema
Kauli ya Dk Bashiru imekuja siku chache baada ya Rais
mstaafu, Benjamin Mkapa kutaka Serikali itambulishwe kuwa ya CCM na si ya mtu.
Mkapa alitoa kauli hiyo katika mkutano wa viongozi wastaafu
ulioandaliwa na Rais Magufuli Ikulu ya Dar es Salaam
Rais huyo wa Awamu ya Tatu alisema angependa kusikia zaidi
Serikali ikijitambulisha kama Serikali ya CCM hasa kwa mawaziri
“Ni Serikali ya CCM inaongozwa na Rais wetu Magufuli lakini
naye ni Rais wa CCM na CCM ndiyo iliyompa urais. Kwa hiyo hii ya kusema mimi,
mimi, aah! Ni Serikali ya CCM, itajenga hamasa ya kuhakikisha inachaguliwa
tena,” alisema Mkapa
Hoja hiyo inashabihiana na ile iliyotolewa hivi karibuni na
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad akiwa
New York, Marekani
Akizungumzia mafanikio ya malengo ya maendeleo endelevu
(SDG), Profesa Assad alisema yatategemea kuimarishwa kwa mifumo ya taasisi na
si viongozi wenye nguvu
Profesa Assad akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Redio Umoja
wa Mataifa alisema, “Tumekuwa na ‘strong personalities’ (watu wenye nguvu)
badala ya kuwa na ‘strong institutions’ (taasisi zenye nguvu.”
Dk Bashiru katika mkutano na waandishi jana alisema,
“Tumetoka katika zama za kusifu mtu, Tunapomtumia Rais Magufuli, ni kiongozi
nyuma, yake kuna umma wa wanachama na wananchi. Lakini ili umma huo uwe na
mwelekeo anakuwepo kiongozi,” alisema
Katibu mkuu huyo alisema, “Kwa hiyo Rais Magufuli ukimtaja,
zungumza kama mwenyekiti wa CCM iliyowahi kuongozwa na Mwalimu Nyerere, Mzee
Mwinyi, Mzee Mkapa, Mzee Kikwete naye atakuwa Mzee Magufuli.”
CCM kuachana na siasa za kusifu mtu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 13, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment