HOSPITALI ya rufani ya mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi), imetoa
tahadhari kwa umma kuhusu kuwapo kwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa ambao hadi sasa
umesababisha vifo vya watu wanne katika kipindi kisichozidi siku 60.
Tahadhari hiyo ilitangazwa jana, na Ofisa afya wa hospitali
hiyo, Dk. Jonas Mcharo, wakati akizungumzia mlipuko wa ugonjwa huo katika
Wilaya ya Moshi.
“Kichaa cha mbwa ni ugonjwa hatari sana na virusi vya ugonjwa
huo husababisha uvimbe kwenye ubongo (encephalytis). Virusi hivi vinaweza
kutokea kwa binadamu na wanyama, lakini ni mara chache hutokea kwa wanyama.
Mpaka sasa kuna watu watatu wamefariki kwa ugonjwa huo na mmoja alishambuliwa
na paka,” alisema.
Watu hao wanadaiwa kufariki dunia wakati wakipatiwa matibabu
katika Hospitali ya Rufani ya KCMC, baada ya kung’atwa au kuumwa na mbwa wenye
ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, kwa kawaida chanjo ya kichaa
cha mbwa iliyothibitishwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na
Wazee na Watoto kwa ajili ya huduma hiyo ni Anti-Rabies, ambayo awali ilikuwa
ikihifadhiwa katika minyororo baridi kwenye hospitali za mkoa,
Inelezwa kuwa kichaa cha mbwa kinaweza kusambazwa kwa mate ya
wanyama wakiwamo paka, popo, ng'ombe, mbweha, fisi na wengine.
Moja ya dalili za ugonjwa huo ni maji ya bomba yanapofunguliwa
mgonjwa huogopa na akionyeshwa kikombe cha maji anaweza kukitupa, dalili
nyingine ni kushindwa kula chakula na wakati mwingine katika hatua za mwisho
mgonjwa hutoka udenda uliochanganyika na damu.
Dk. Mcharo alisema wakazi 64 wa Kijiji cha Mawala, Kata ya Kahe,
Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, wamejitokeza kwa hiari kupatiwa chanjo ya
kujikinga na ugonjwa huo.
TAHADHARI KICHAA CHA MBWA
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 07, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment