Mjadala uliosababisha baadhi ya wabunge
kususia kikao juzi, umemfanya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutoa ya moyoni
wakati akihitimisha hotuba ya bajeti ya ofisi yake jana
Majaliwa amesema kwamba mjadala ulioibuka
juzi kuhusu
Muungano haukuwa na afya na hatarajii kuona hali hiyo ikijirudia
Juzi wabunge wa upinzani kutoka Zanzibar
walitoka ukumbini baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu kuagiza mjadala
usio na afya kwa Muungano usijadiliwe hadi atakapojibu mwongozo ulioombwa na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge), Jenista Mhagama
Jenista aliomba mwongozo wa Spika akitaka
kiti kutenda haki kuzuia mjadala usio na afya bungeni ukiwemo wa Muungano
“Mheshimiwa Spika, nieleze masikitiko yangu
juu ya mjadala ulioendelea jana, sikuridhika na mjadala wa jana,” alisema
Majaliwa wakati akianza kuhitimisha hotuba yake
“Najua ziko hoja lakini mjadala wa jana
(juzi) kwa namna nilivyojifunza ni mgogoro wa mtu na mtu, kundi na kundi, jambo
ambalo halileti tija wala afya hapa kwetu.”
Majaliwa alisema anatambua kuwa yapo
mapungufu, lakini viongozi wote wameapa kuusimamia Muungano na kwamba jukumu la
wengine ni kuunga mkono ili kuulinda
“Tunajua kwamba kutokana na kuingia
madarakani na Serikali ya sasa ina miaka miwili, yapo maboresho na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, yapo maboresho. Maboresho haya yanaweza kuathiri mfumo
wa kawaida ambao tulianzanao na ambao tunaumaliza kupitia vikao tulivyo navyo,”
alisema
Alisema hawazuii mbunge kuuliza jambo ili
apate ufafanuzi, lakini pia “haturuhusu mtu na mtu watumie Bunge kupotosha
ukweli wa mambo”. Awali juzi, mbunge wa Chambani (CUF), Yusuf Hussein Salim
alisema changamoto za Muungano hazijatatuliwa akitoa mfano wa sukari ya
Zanzibar kuzuiwa kuuzwa Tanzania Bara, kauli iliyoibua mjadala
Na Majaliwa alidokezea suala hilo akisema
suala hilo lilitokana na sukari
Waziri mkuu alisema chanzo cha malumbano ni
suala la uagizaji sukari kutoka nje ya nchi ili kufidia upungufu uliopo nchini
Alisema katika kutimiza azma hiyo, Serikali
haiangalii kama mwagizaji ametoka Tanzania Bara au Zanzibar
Waziri Mkuu alitoa mfano, akisema mwaka 2016
upungufu uliojitokeza ulikuwa tani 140,000 lakini waagizaji waliopewa vibali
walikuwa wawili kutoka Zanzibar, watatu kutoka Bara na kiwanda cha sukari cha
Mahonda kilipewa kibali cha kuagiza tani 390
Alisema mwaka 2017, upungufu ulikuwa tani
140,000 na waliopewa vibali walikuwa wawili kutoka Zanzibar na wawili kutoka
Bara, lakini kwa mwaka huu upungufu ni tani 135,000
Waziri mkuu alisema tofauti na awali, safari
hii waliopewa vibali ni wenye viwanda ili waagize sukari kutoka nje
“Kwa hiyo, jambo hili la sukari lisivuruge
Muungano wetu,” alisema Majaliwa
Alisema nia ya Serikali ni kuzalisha sukari
ya kutosha ili Taifa lijitegemee
Majaliwa aliwataka mawaziri wa biashara wa
Zanzibar na Bara wawe makini ili sukari inayoagizwa nje isije kufurika katika
soko la ndani kwa sababu gharama za uzalishaji sukari ya ndani ni kubwa
Alisema viwanda vilivyopo ni sita, vitano
vikiwa Bara na kimoja Zanzibar, lakini havina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya
bidhaa hiyo.<
Demokrasia nchini
Baada ya kuhitimisha hotuba hiyo, mawaziri
walijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na wabunge
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama akijibu hoja za wabunge waliochangia hotuba
hiyo alimuomba Msajili wa Vyama vya Siasa kuendelea kuchukua hatua stahiki kwa
vyama vyote ambavyo havitaki kufanya shughuli zake kwa kufuata sheria na utaratibu
ili kusaidia mfumo wa vyama vingi uwe halisia unaoendana na matakwa ya kisheria
Kuhusu kuzuiwa maandamano, Mhagama alisema
wabunge wa upinzani wamelalamika kwamba yanazuiwa wakati ni suala la kikatiba
Alisema maandamano yanaratibiwa kwa sheria
ya usalama chini ya polisi, na Katiba haiwezi kuchukuliwa tu kuruhusu
maandamano bila sheria kufuatwa
“Niulize tu, tukiamka hapa siku moja asubuhi
kila mtu aamue kuandamana kwa sababu Katiba imesema, nadhani haitakuwa sawa.
Naomba vyama viheshimu Katiba na sheria,” alisema Mhagama
Kuhusu fedha nyingi kutumika katika uchaguzi
mdogo, alisema hakuna demokrasia isiyo na gharama
“Kama jimbo la uchaguzi lipo wazi lazima
tufanye uchaguzi, ndiyo maana nasema ni gharama ya demokrasia,” alisema
Operesheni uvuvi haramu
Naye Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,
Luhaga Mpina aliomba kibali kwa Waziri Mkuu na kwa Spika ili wakubali aendeshe
semina Aprili 21 aeleze jinsi gani rasilimali zilizoko katika sekta ya uvuvi
zinavyofujwa na watu wasilolitakia mema Taifa
“Lakini yapo mambo madogo ambayo
yameshauriwa na wabunge katika uboreshaji na mimi sina tatizo na uboreshaji.
Ndiyo maana katika Bunge lile nilisema mbunge yeyote mwenye hoja, mwenye jambo
lolote atuletee sisi tutachukua hatua,” alisema
Alisema tayari wamewasimamisha kazi
watumishi tisa waliohusika kwa namna moja kuhujumu au kujinufaisha binafsi
katika operesheni hiyo
Alisema ametoa maelekezo kwa maofisa wake
kuacha kuwakamata watu wanaobeba samaki kwa ajili ya kitoweo cha nyumbani ambao
awali, walikuwa wakikamatwa katika mabasi
Hata hivyo, aliwaonya watu kutotumia mwanya
huo kutumia mabasi ya abiria kwa ajili ya kufanya biashara
Mauaji, utekaji
Kuhusu matukio ya utekaji, Waziri wa Mambo
ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba aliagiza kufanyika uchunguzi wa ndani ili kupata
taarifa na wataendelea kutoa taarifa kadri zitakavyopatikana.
Mjadala Muungano wamkwaza waziri Mkuu Kasim Majaliwa
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 11, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment