Urais wa Trump watikiswa mahakamani


Kesi mbili zilizosikilizwa katika mahakama tofauti dhidi ya washirika wa zamani wa karibu wa Rais Donald Trump zimeibua vuta nikuvute ya kisheria baada ya mmoja kukiri kuwa na hatia na mwingine kukutwa na hatia hivyo kumweka matatani mkuu huyo wa nchi

Walioutikisa urais wa Trump ni meneja wake wa zamani wa kampeni, Paulo Manafort ambaye amepatikana na hatia katika mashtaka manane kati ya 18 ya udanganyifu wa kodi na masuala ya kibenki; na mwanasheria binafsi wa zamani, Michael Cohen aliyekiri kuwa na hatia kwa mashtaka manane, yakiwamo sita ya udanganyifu wa kodi na benki na mawili ya kufadhili kampeni za uchaguzi kinyume cha sheria

Mbaya zaidi, mwanasheria huyo wa zamani wa Trump aliithibitishia mahakama kwamba alikiuka sheria kwa maelekezo ya mgombea huyo wa urais ambaye sasa ni Rais

Hili ni pigo kubwa kwa Trump baada ya kuhusishwa na mtu ambaye alikuwa akimwamini kwa zaidi ya muongo mmoja. Cohen aliyeeleza kuwa ni mtu wa karibu wa Trump alisema alikuwa akihusika kutatua matatizo yake

Kwa maelezo hayo, Cohen kwa hakika sasa anaweza kuwa chanzo cha matatizo makubwa kwa Trump kwani alikiri kuwa alilipa dola za Marekani 130,000 na 150,000 kwa wanawake wawili ili kuwaziba midomo kuhusu uhusiano wao na Trump kwa maelekezo ya mgombea huyo

“Rais alisema akiwa katika ndege ya Air Force One kwamba hajui kuhusu muamala wa malipo ya dola 130,000, lakini sasa tunajua ukweli kutoka kwa Michael Cohen, na tunaweza kusema kuwa Rais wa Marekani alidanganya wananchi wa Marekani wakati alikuwa ndani ya ndege ya wananchi wa Marekani,” mahakama ilielezwa

Hata hivyo, Cohen amekata rufaa katika mahakama ya Manhattan dhidi ya madai yanayomkabili kwamba alikiuka sheria za uchaguzi na kudai kuwa alifanya hivyo kwa maelekezo ya “mgombea”, kwa lengo la kuhakikisha uchaguzi unakuwa salama

Katika kipindi cha miaka 10 ya utumishi wake akiwa mwanasheia wa Rais, Cohen anadaiwa kuandaa malipo kwa mwigizaji wa filamu za ngono, Stormy Daniels mwaka 2016

Mei mwaka huu, Trump alikiri kumpa Cohen fedha za malipo ya kutaka kumnyamazisha mwigizaji huyo kuhusiana na suala la kuwa na uhusiano na mlimbwende huyo siku kadhaa kabla ya kuanza kwa uchaguzi mkuu

Ingawa katika siku za karibuni, Trump amekana kufahamu muamala wa malipo ya dola za Marekani 130,000 kama sehemu ya malipo ambayo hayajabainishwa

Mwezi uliopita ilifahamika pia kuwa Cohen alimrekodi kwa siri Trump walipokuwa wakijadiliana kuhusu ununuzi wa haki za umiliki wa mcheza filamu za ngono, Karen McDougal ikiwamo hadithi yake kutoka kwa kampuni dada la jarida la Enquirer

Malipo yafanywayo kwa siri kwa niaba ya mwanasiasa au mgombea yeyote yanaweza kuchukuliwa kama ukiukwaji wa sheria za kampeni Marekani

Urais wa Trump watikiswa mahakamani Urais wa Trump watikiswa mahakamani Reviewed by KUSAGANEWS on August 23, 2018 Rating: 5

No comments: