MTU aliyefahamika kwa jina la Castory Mwaituro, amefariki
dunia baada ya kushambuliwa na mnyama aina ya kiboko alipokuwa anavua samaki
kwenye bwawa ka Mtera
Mwaituro alikumbwa na mkasa huo Jumatatu wiki hii kwenye
bwawa hilo katika kijiji cha Mnadani Mabati, kata ya Izazi wilayani Iringa
Akizungumza na Nipashe juzi, Mwenyekiti wa Kijiji cha
Mnadani, Yared Mlula, alisema viboko hao wamekuwa wakiwadhuru wavuvi ambao
wamekuwa wakifanya shughuli hiyo kwenye bwawa hilo.
Kutokana na tukio hilo, Diwani wa Izazi, Golden Mzinga,
ameiomba serikali kuwavuna viboko hao ambao wamekuwa wengi, hivyo kusababisha
wavuvi kushindwa kuvua samaki.
Alisema wananchi wengi katika kijiji hicho ni wavuvi ambao
wanategemea vipato vyao kutokana na shughuli hiyo, hivyo kuwapo kwa viboko
kwenye bwawa hilo kumekuwa kikwazo kwao.
Alisema tukio la kuuawa kwa Mwaituro ni la tatu katika
kipindi kifupi. Aliwataja wengine waliouawa kuwa ni Patrick Kibehe na Sulupia
Longo.
Kwa mujibu wa diwani huyo, viboko hao wanatesa wananchi wa
kijiji hicho hatua ambayo inasababisha kupoteza nguvu kazi
Naye mkazi wa kijiji hicho, Emmanuel Gama, kutoka kitongoji
cha Mabatini, ambaye alikuwa na Mwaituro wakati mkasa huo ukitokea, walikuwa kwenye
mtumbi wakati wakikagua nyavu na ndipo kiboko huyo alipotokea na kuwashambulia.
“Wakati tunaendelea kukagua nyavu, ghafla kiboko aliibuka na
kupiga mtumbwi juu na tukaangukia kwenye maji na kuanza kuogelea. Baada ya muda
tulichoka na kiboko alimfuata mwenzangu na kuzama naye majini,” alisema.
Hata hivyo, alisema hakukata tamaa kwa kuwa alimfuata rafiki
yake na mtumbwi mwingine kwa lengo la kumuokoa na kumkuta akiwa katika hali
mbaya. Alisema alimchukua kumpeleka hospitalini lakini alipoteza maisha wakiwa
njiani
Akizungumzia changamoto hiyo, Ofisa Wanyamapori wa Wilaya ya
Iringa, Fatuma Juma, alisema wamesharipoti katika idara ya wanyamapori kuomba
wawavune viboko hao ili kupunguza matukio ya watu kupoteza maisha
Auwawa na Kiboko akivua Samaki
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 23, 2018
Rating:

No comments:
Post a Comment