Mbunge wa Nzega (CCM), Hussein Bashe amewahakikishia wananchi wa
Tanzania kuwa hoja yake aliyoiwakilisha kwa Katibu wa Bunge kuwa haiwezi
kukwamishwa na jambo lolote kwa madai hakuna kisichojulikana kinachoendelea
kutoka katika nchi.
Bashe ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa
anazungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuelezea
sababu zilizompelekea yeye kama Mbunge kuandika barua ya kutaka kuundwe kwa
kamati ya uchunguzi dhidi ya matukio mbalimbali yanayoonesha kutishia umoja,
usalama na mshikamano wa taifa la Tanzania.
"Madhumuni ya kikatiba ya Chama cha Mapinduzi (CCM)
ni kuwasemea wananchi, kuwatetea kwa hiyo natimiza wajibu wangu kama Mbunge
sioni kama nitapoteza Ubunge wangu katika hili.
"Mimi ninaamini nitapoteza ubunge wangu kwasababu
zifuatazo, endapo nitashindwa kutimiza wajibu wangu ndani ya Bunge, nikishindwa
kutimiza wajibu wangu ndani ya Jimbo langu kwa maana nimeshindwa kuisimamia
serikali katika kuleta maendeleo, nimeshindwa kutimiza ahadi wakati wa uchaguzi
katika jimbo langu na mwisho wanaccm watakaposema kwenye mchakato wa
kidemokrasia wa kura kwamba Hussein wewe hapana.
"Mimi ni muumini wa kiislamu ninaamini kila binadamu umauti
utamfika (kifo) na chochote kitakachonifika ni kile ambacho amekipanga Mwenyezi
Mungu lakini sina hofu yeyote kwasababu hili sio taifa la namna hiyo.
"Nikiwa kama Hussein sidhani hii hoja kama inakwenda
kukwama kwasababu unapoikwamisha hoja unapaswa kusema unaikwamisha kwa kutumia
misingi gani kama watu wanaamini kwa kila kinachotokea ndani ya ardhi ya
Tanzania sioni kama itakwama.
"Bunge limeshafanya maamuzi mbalimbali juu ya masuala
mbalimbali katika rekodi ya nchi hii, kwa hiyo mimi nadhani ni muhimu tukatoa
fursa jambo hili lifike Bungeni na likifika huko kama litakataliwa basi tujue
ni kwasababu zipi na kama nilivyofanya kuwaambia watanzania ndivyo hivyo
nitarudi kuwaambia limekataliwa kwasababu zipi na hapo tutajadili hatua za
kufanya".
Kwa upande mwingine, Bashe amesema anasubiria majibu ya barua
aliyotuma kutoka kwa Katibu wa Bunge Pamoja na Katibu Chama cha Mapinduzi (CCM)
ambayo ameeleza dhamira na nia yake huku akisisitiza zaidi kuwa jambo hilo
hajalifanya kwa mihemuko (kukurupuka) bali amefanya kwa umakini wa hali ya juu
na utafiti wa kutosha.
Bashe: Madhumuni ya kikatiba ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ni kuwasemea wananchi,
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 08, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment