Padri Raymond Mayanga wa Parokia
ya Yohane Mbatizaji Luhanga amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kumsaka
mtu aliyempiga risasi mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafishaji (NIT),
Akwilina Akwilini, kumweka wazi ili awaombe radhi Watanzania.
Akizungumza katika ibada ya kuaga
mwili wa mwanafunzi huyo inayofanyika katika viwanja vya NIT, Mabibo, Padri
Mayanga amesema mtu huyo hata akifungwa miaka 30 hadi 40, Akwilina hatarudi
“Awe amefanya kwa nia nzuri au mbaya
vyombo vinavyohusika vikimaliza taratibu zake kama ni kupitia televisheni ama
nini huyu mtu aombe msamaha, vinginevyo hatutafika mbali. Leo kwa Akwilina
huenda mwingine,” amesema.
Naye mwakilishi wa familia ya
Akwilina, Aloyce Shirima amesema, “Tunaomba mtufikishie salamu kwa Rais John
Magufuli kuwa wale wote waliofanya kitendo hicho wachukuliwe hatua
stahiki. Taifa haliwezi kuendelea kwa kuondokewa na wasomi kizembe.
“Akwilina ni mtoto wa sita katika
familia ya watoto nane wa mzee Akwilini na ni mtoto pekee aliyependa
elimu katika familia hiyo.”
Rais wa Serikali ya wanafunzi NIT,
Mchunja Othman amesema, “Alikuwa mcheshi asiyejua kununa. Tunaiomba Wizara ya
Mambo ya Ndani kuhakikisha inalisimamia hili ili haki itendeke. Hii inatupa
fursa ya kujifunza sisi kama binadamu maisha yetu siyo ya kudumu hivyo
tutende mema.”
|
Padri ataka aliyempiga risasi Akwilina awekwe wazi, awaombe radhi Watanzania
Reviewed by KUSAGANEWS
on
February 22, 2018
Rating:

No comments:
Post a Comment