Leo wakati mkutano wa saba , kikao
cha 40 kikiendela bungeni Dodoma umeibuka mjadala wa dawa za kulevya aina bangi
baada ya baadhi ya wabunge kusema kuna vitendo vinavyofanywa na baadhi ya
polisi nchini vinatokana na polisi hao kuwa wamelewa bangi.
Katika mjadala huo Mh Spika Job
Ndugai naye alichomekea kuwa huwa anasikia watu wanasema bangi zinaongeza
nguvu, hivyo naye alitaka kujua hizo bangi zinaongeza nguvu za aina gani, huku
akiwauliza wabunge ambao wanatokea maeneo ambayo bangi imekuwa ikiripotiwa
sana.
Kufuatia mjadala huo kuendelea
alisimama Mbunge Esther Matiko Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara na kusema
yeye mwenyewe huwa anaona polisi wakichoma bangi katika maeneo hayo na kudai
huenda baadhi ya vitendo vinavyofanywa na polisi wetu ni kutokana na kuathirika
na moshi wa bangi wakiwa wanachoma bangi hizo. Lakini katika ufafanuzi wa Naibu
Waziri wa Afya alisema polisi hao wao huwa hawaathiriki na moshi huo.
"Jamani tunapojadili juu ya
suala la madawa ya kulevya si jambo la mzaha, ni kwamba polisi wanapokwenda
kuchoma bangi mashambani huwa wanajifunika vifaa maalum lakini hata kama
hawajifuniki vifaa hivyo bado ile bangi ikiingia kwenye miili yao itaondoka
ndani ya siku 30 kwani inageuka na kuwa chumvi na kutoka kwa njia ya mkojo na
jasho. Lakini kwa watu ambao wanatumia kila siku yaani leo, kesho, kesho kutwa
na kuendelea wao wanakuwa ni clonic wa dawa hizo" alisema Kigwangalla
Licha ya Naibu Waziri wa Afya kutoa
ufafanuzi juu ya uchomaji wa bangi lakini Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana,
Ajira na Walemavu, Jenista Joakim Mhagama alisimama na kutoa ufafanuzi wake pia
akisema kuwa polisi hawajaathirika na bangi kutokana na namna ambavyo huwa
wanachoma bangi hizo kwa kufuata utaratibu mzuri.
"Mh. Spika vikosi vya polisi
vinavyofanya utekeketezaji wa bangi, zipo njia nyingi wanatumia kuteketeza
bangi hizo, kwanza wakiwa wanafanya zoezi hilo huwa wanaangalia uelekeo wa
upepo lakini pia maandalizi mengine ya vifaa vyao vya uteketezaji wa bangi,
aina ya mafuta yanayotumia kwenye kuchomea bangi hizo vinawafanya kuwa salama
kabisa, kwa hiyo siyo kweli kwamba likitokea tatizo kwenye jeshi la polisi
kwamba polisi wetu wameathirika na matumizi ya bangi, kwani polisi wetu ni
weledi na wanafanya kazi kwa kufuata utaratibu na sheria" alisisitiza
Mhagama
Kwa kumalizia mjadala huo Spika wa
Bunge, Job Ndugai alisema kuwa nchi nzima na viongozi wamesikia juu ya jambo
hilo hivyo wanapaswa kuwa makini katika utekelezaji wa mambo hayo.
MJADALA WA BANGI WATIKISA BUNGE,POLISI WATAJWA
Reviewed by KUSAGANEWS
on
June 02, 2017
Rating:

No comments:
Post a Comment