JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) imelaani migogoro katika ndoa inayosababisha ongezeko la
matukio ya mauaji miongoni mwa wanandoa hali inayotishia ustawi wa watoto na
kuchangia ongezeko la watoto waishio katika mazingira magumu.
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya
Wazazi kitaifa, Burhan Rutta alisema, Jeshi la Polisi na jamii kwa jumla
zikiwamo taasisi za dini, waongeze ushirikiano kubaini dalili za maisha
hatarishi ili kunusuru mauaji kutokea. Wakati akisema hivyo, Mkurugenzi
Mtendaji wa Chama cha Wajane Tanzania (Tawia), Rose Sarwatt alisema jana kuwa,
vurugu na mauaji miongoni mwa wanandoa yanayoelezwa kusababishwa na wivu wa
mapenzi, ni matokeo ya baadhi ya watu kuingia katika ndoa kwa kuvutwa na
maslahi binafsi, badala ya upendo.
“Wengi siku hizi wanaingia katika
ndoa wakisukumwa na maslahi binafsi na kwamba kuna kitu anakwenda kukipata.
Mambo yakiwa tofauti, anaamua kuishi na kufanya lolote kwa sababu haoni kutimia
kwa matarajio yake,” alisema Rose. Akaongeza kuwa, kinachoelezwa kuwa wivu wa
mapenzi, kimeficha mambo mengi ndani yake likiwamo hasa la mtu kukosa yale
aliyotarajia kuyakuta hasa mali na tamaa na mvuto wa mwonekano wa nje. Naibu
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM alisema: “Jambo hili la ukatili na hata
mauaji miongoni mwa wanandoa lipigiwe kelele na watu wote.
vyombo vya dola viwatafute na
kuwakamata wanaofanya mambo hayo na kukimbia ili wapatikane na kufikishwa mbele
ya sheria.” Pia aliitaka jamii ya Watanzania kubadilika na kuutanguliza utu,
badala ya maamuzi mabovu yanayosababisha vifo na kuwaweka watoto katika maisha
magumu huku taifa likipoteza nguvu kazi. Hivi karibuni mkazi wa Kijiji cha
Muriti wilayani Ukerewe, Melikiad Misana (50) alifariki dunia wakati
akikimbizwa hospitali baada ya mkewe Bukherehere William (25) kumchoma na kitu
chenye ncha kali mgongoni.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza,
Ahmed Msangi alisema tukio hilo lilitokea baada ya mwanaume huyo kumjeruhi
mkewe huyo kwa kuchoma na kitu chenye ncha kali kwenye mikono yake na tumboni
kiasi cha kusababisha utumbo wa mwanamke huyo, kutoka nje. Tukio hilo lilikuja
siku chache baada ya mkazi wa Kanyerere jijini Mwanza, Maximilian Ndegere (40),
kumuua mkewe Teddy Patrick (38) kwa risasi na kisha yeye kujiua.
JUMUIYA YA WAZAZI YALAANI MAUAJI YA WANANDOA
Reviewed by KUSAGANEWS
on
June 02, 2017
Rating:

No comments:
Post a Comment