Jeshi la polisi mkoani
Singida,linamshikilia mkulima mkazi wa Mitunduruni mjini hapa, Mariamu Juma
(21), kwa tuhuma ya kuchoma nyumba moto na kuteketea pamoja na mali zote
zilizokuwemo.
Kwa mujibu wa kamanda Jeshi la
Polisi mkoa wa Singida, ACP Debora Magiligimba, kitendo hicho kimechangiwa na
wivu wa kimapenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake, Kamanda Magiligimba,alisema kuwa tukio hilo limetokea Mei 30
mwaka huu saa 11.40 jioni, huko maeneo ya Mwenge tarafa ya Mungumaji Manispaa
ya Singida.
Akifafanua, alisema kuwa siku ya
tukio mtuhumiwa alienda kwenye nyumba aliyopanga mpenzi yake Benardo Mabula,
ambayo inamilikiwa na Omari Hamisi (35) katika maeneo ya Mwenge mjini hapa.
“Uchunguzi wa awali wa Jeshi la
Polisi umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo, ni wivu wa kimapenzi. Mtuhumiwa
Mariamu alipoingia kwenye chumba cha rafiki yake wa kiume (Mabula),aliwasha
moto kwa kiberiti kwa lengo la kuchoma vifaa vya mpenzi wake,” alisema na
kuongeza;
“Lakini moto huo ulisambaa vyumba
vyote vya nyumba hiyo na kuteketeza kila kitu.Hadi sasa thamani ya nyumba na
mali iliyoteketea, bado haijafahamika.”
Kamanda huyo alisema kuwa baada ya
uchunguzi kukamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma
inayomkabili. Mpenzi wa mtuhumiwa Mariamu,amefanikiwa kutoroka na kukimbilia
kusikojulikana.
“Jeshi la Polisi mkoani hapa,linatoa
wito kwa wananchi wote hasa familia zenye migogoro ya ndoa,wafike ofisi zetu za
dawati la jinsia na watoto zilizopo kila wilaya, ustawi wa jamii na viongozi wa
dini, ili waweze kusikilizwa matatizo yao, badala ya kujichukulia sheria
mkononi,” alisema Magiligimba.
Katika hatua nyingine, Kamanda huyo
alisema vikongwe wawili wamefariki dunia papo hapo, baada ya kuangukiwa na
ukuta wa nyumba iliyojengwa kwa tofali za tope na kuezekwa kwa bati.
Magiligimba alisema vikongwe hao na
watu wengine, walikuwa kwenye nyumba hiyo, kushiriki mazishi ya Mwajuma Mwendo
aliyefariki Mei, 28 na kuzikwa kesho yake.
Aliwataja vikongwe hao kuwa ni Nzitu
Mkumbo (80) mkulima kwa kijiji cha Mwangeza ambaye alivunjika miguu yote na
mkono wa kushoto.Mwingine ni Kimwana Kingu (90) mkulima wa kijiji cha
Mazangila, ambaye alivunjika mguu wa kulia na kujeruhiwa vibaya mguu wa
kushoto. Vijiji hivyo vipo wilaya ya Mkalama.
Aliwataja waliojeruhiwa katika ajali
hiyo ni Fatma Alli (70), Zena Ntoga (40), Kimwana Mohammed (70), Gyoli Kingu
(45), Habiba Hussein (40) na Sophia Mashimba (50).
Alisema chanzo cha tukio hilo ni
uchakavu wa nyumba hiyo iliyoanguka baada kupigwa na upepo mkali na kusababisha
ukuta wa ndani uliotenganisha chumba na sebule, kuanguka.
“Jeshi la polisi mkoa wa
Singida,linatoa wito kwa wananchi wote wawe na utaratibu wa kukarabati nyumba
zao mara kwa mara.Pia tunawashauri wapande miti kwa wingi kuzunguka maeneo ya
makazi yao,” alisema kamanda Magiligimba.
BINTI ACHOMA MOTO NYUMBA AKIMKOMESHA MPENZI WAKE HUKO SINGIDA
Reviewed by KUSAGANEWS
on
June 02, 2017
Rating:

No comments:
Post a Comment