Zitto Kabwe 'Akaabwa Koo' Zanzibar......Apewa Siku 14 za Kuomba Radhi Kwa Kumhusisha Dr. Shein na Makosa ya Uhaini

Mbunge wa Kigoma Mjini  kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo,  Zitto Kabwe, amepewa siku 14 kufuta kauli yake na kuomba radhi kwa kumhusisha rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na makosa ya uhaini.

Msimamo huo ulitolewa na wagombea wawili wa nafasi ya urais wa Zanzibar, Juma Ali Khatib (Tadea) na Soud Said Soud, walipokuwa wakizungumzia kauli ya Zitto kudai haikuwa sahihi kwa Rais wa Zanzibar kubakia madarakani wakati serikali yake imefikia ukomo wake Novemba 2, mwaka huu.

Soud alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar Kifungu cha 28 (1)(a), Rais Shein ni Rais halali wa Zanzibar  na atabakia madarakani hadi atakapochaguliwa rais mpya kwenye uchaguzi wa marudio.

Alisema kuwa Dk. Shein alichaguliwa na wananchi wa Zanzibar na haikuwa haki kwa Zitto kumhusisha na makosa ya uhaini kwa kuendelea kubaki madarakani kwani  yuko kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. 
 
"Zitto Kabwe afute kauli yake na kuwaomba radhi wananchi wa Zanzibar ndani ya siku 14  na asipofanya hivyo tutamfungulia mashitaka." alisema Soud pia Mwenyekiti wa Chama cha AFP.

Katika sakata hilo, Juma Ali Khatib, alisema tayari ameanza kutafuta namna ya kuwasiliana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuwasilisha malalamiko yake dhidi ya Zitto kwa kumhusisha na makosa ya uhaini Rais wa Zanzibar.

Alisema iwapo Bunge litashindwa kumchukulia hatua za kinidhamu Zitto, yeye atalazimika kufungua kesi kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar kupinga kauli ya Zitto.

Khatib alisema Zanzibar ni nchi na Rais wa Zanzibar lazima apewe heshima yake kwa sababu kuendelea kuwepo kwake madarakani ni matakwa ya Kikatiba.

"Kumdhalilisha Rais wa nchi ni sawa na kutudhalilisha wananchi wake, rais anashauriwa na vyombo vingi vya sheria hivyo hawezi kuvunja Katiba," alisema Khatib
 
Viongozi hao si wa kwanza kujitokeza kumtetea Rais wa Zanzibar  kwani walitanguliwa na aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Katiba, Simai Mohamed Said, tangu Zitto alipotoa kauli kuwa Zanzibar haina rais na kuendelea kubakia madarakani Rais Shein ni sawa na kufanya uhalifu wa uhaini.

Katika mkutano wake na wandishi wa habari hivi karibuni, Zitto alisema kwa sasa Zanzibar haina serikali na mtu yoyote anayejiita rais wa Zanzibar  kikatiba amepindua nchi na katika hali ya kawaida anapaswa kushitakiwa kwa uhaini.
Mpekuzi blog
Zitto Kabwe 'Akaabwa Koo' Zanzibar......Apewa Siku 14 za Kuomba Radhi Kwa Kumhusisha Dr. Shein na Makosa ya Uhaini Zitto Kabwe 'Akaabwa Koo' Zanzibar......Apewa Siku 14 za Kuomba Radhi Kwa Kumhusisha Dr. Shein na Makosa ya Uhaini Reviewed by KUSAGANEWS on November 28, 2015 Rating: 5

No comments: